Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akitimiza siku 100 ofisini tangu kuanza kwa muhula wake wa pili, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa hakitambui mamlaka yaliyopo madarakani na kinadai uchaguzi mkuu mpya.
Akizungumza katika mahojiano maalum na BBC Swahili leo Februari 10, 2026, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, ametoa msimamo mkali wa chama hicho akidai kuwa mchakato wa Oktoba 29, 2025, haukuwa uchaguzi halali.
Heche amebainisha kuwa CHADEMA haihesabu wala kuitambua kalenda ya siku 100 za Rais Samia kwa hoja kuwa viongozi waliopo ofisini wamejipachika madarakani badala ya ridhaa ya wapiga kura.
“Sisi hicho kinachoitwa siku 100 hatukitambui. Msimamo wetu wa chama kuhusu kinachoitwa uchaguzi uko wazi kwamba uchaguzi haukufanyika. Hatutambui viongozi walioko kwenye madaraka kwa sababu ni watu wamejipachika kinyume cha katiba ya nchi yetu ibara ya nane”, amesisitiza Heche.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa maridhiano na mchakato wa Katiba Mpya, Heche ameweka wazi kuwa mazingira ya sasa hayaruhusu mazungumzo yoyote. Amebainisha kuwa viongozi wa CHADEMA hawawezi kufanya maamuzi ya maridhiano wakati Mwenyekiti wao, Tundu Lissu, bado yuko gerezani na mikutano ya vikao vikuu vya chama imezuiliwa.
“Unajua haya mambo tulisema mwanzo kwamba jamani eeh, msiende kwenye mazingira haya yatatuletea shida kubwa. Sasa hayo maridhiano unayafanyaje? Jambo la kwanza sisi kwetu, mimi binafsi kama John Heche, siwezi kuamua jambo bila chama kukaa vikao na kuzungumza. Vikao vya chama chetu vinavyoweza kufanya maamuzi kama makubwa ni kikao cha kamati kuu na baraza kuu na mkutano mkuu ambavyo kwa sasa vimezuiliwa kinyume cha utaratibu wa sheria”, ameeleza Heche na kuongeza,
“Watu wamepoteza ndugu zao, hawajapewa hata miili kuzika ndugu zao. Watu walioumiza watu…hawajawajibishwa. Sasa unafanya maridhiano ya aina gani?”
Kama njia ya kuiondoa nchi katika mkwamo wa kisiasa, Heche ametoa ushauri kwa Rais Samia kuwa hatua pekee ya busara ni kuridhia kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwingine. Amesema hiyo ndiyo njia rahisi na ya kistaarabu itakayowaruhusu wananchi kuchagua kiongozi wanayemtaka kwa njia ya kidemokrasia na kurejesha utulivu wa kweli nchini Tanzania.