Latest Posts

KESI YA LISSU, PINGAMIZI LA JAMHURI LAGONGA MWAMBA

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam mapema leo, Jumatatu Oktoba 13.2025 imetoa ‘uamuzi mdogo’ kufuatia pingamizi lililokuwa limewekwa mwishoni mwa juma lililopita na upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Tundu Lissu

Pingamizi hilo lilitokana na mshtakiwa ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo kuomba kielelezo D1 (maelezo ya maandishi ya shahidi wa pili wa Jamhuri Inspekta wa Jeshi la Polisi John Kaaya aliyoandika akiwa kwenye Kituo cha Polisi) cha PW2 ambaye ndiye shahidi, upande wa Jamhuri ulipinga kielelezo hicho kupokelewa Mahakamani hapo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa mshtakiwa hajazingatia taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria pale mshtakiwa anapotaka kumuhoji shahidi kuhusu maelezo aliyotoa hapo awali

Katika kujenga msingi wa pingamizi lao, Mawakili wa Jamhuri Ajuwaye Nzegeli (Wakili wa Serikali Mkuu) na Job Mrema (Wakili wa Serikali Mkuu) waliipitisha Mahakama kwenye marejeo ya mashauri mbalimbali ya aina hiyo yaliyoamuliwa na Mahakama Kuu na Mahakamani ya Rufani, marejeo ambayo katika uamuzi wake Mahakama imesema hoja hiyo haijabishaniwa na pande zote mbili

Katika uamuzi wake, jopo la Majaji watatu (3) wanaosikiliza kesi hiyo wakiongozwa na Jaji Danstan Ndunguru wamesema mshtakiwa amefuata taratibu zote zinazohitajika kisheria katika kuomba kielelezo hicho kupokelewa Mahakamani

Wamesema kwa mujibu wa taratibu za kisheria panapotokea mazingira ya aina hiyo kuna hatua tatu (3) za kufuatwa, kwanza ni shahidi kusomewa maelezo yake, baada ya hapo mshtakiwa atabainisha maeneo anayoona yana ‘kasoro’ kwa ulinganifu ili ayafanyie dodoso na kwamba kwa muktadha wa kesi pingamizi hilo Mahakama imeona kuwa mshtakiwa alibainisha maeneo 45, na jambo la tatu ni kumuhoji mshtakiwa endapo yuko tayari kielelezo hicho kipokelewe Mahakamani na kitumike kama sehemu ya ushahidi wake, hatua ambazo zote zilifuatwa

Kufutia maamuzi hayo ya Mahakama, sasa kielelezo hicho (D1) kinakuwa cha kwanza cha mshtakiwa Tundu Lissu kuwasilishwa Mahakamani hapo, na sasa kesi hiyo inaendelea ambapo mshtakiwa anaendelea kumuhoji maswali ya dodoso (cross examination) shahidi wa pili (2) wa Jamhuri Inspekta wa Jeshi la Polisi John Kaaya.

Jambo TV itaendelea kukuletea kile kinachoendelea Mahakamani hapo kuhusiana na kesi hiyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!