Na; mwandishi wetu
Kesi ya uhaini Na. 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu imeendelea tena leo, Jumatano Februari 18.2026, kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam
Kesi hiyo ya jinai inayosikilizwa mfululizo mbele ya jopo la Majaji watatu (3) wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru imekuja kwaajili ya upande wa Jamhuri kuendelea kuwaleta Mahakamani mashahidi na kutoa ushahidi wao, ikumbukwe kuwa Jamhuri kwenye kesi hii ina mashahidi 30 na vielelezo tisa (9) kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa Mahakamani hapo siku za nyuma, ambapo kati ya mashahidi hao 30, mashahidi 11 ni wa kificho (siri), yaani raia waliopatiwa ulinzi wa utambulisho wao na Mahakama, na mashahidi waliosalia wote si wa kificho ambao kimsingi ni askari kutoka vyombo mbalimbali vya Ulinzi na Usalama Nchini wengi wao wakiwa ni Maafisa wa Jeshi la Polisi,
Mapema Mahakamani hapo upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Renatus Mkude uliieleza Mahakama kuwa leo walitarajia kuwapandanisha kizimbani mashahidi wawili (2), mmoja shahidi wa siri na mwingine ni Askari mpelelezi, lakini alfajiri ya leo wamepokea taarifa kuwa yule shahidi wa pili (Askari mpelelezi) amefiwa na Baba Mkwe wake hivyo ameshindwa kufika Mahakamani na kutoa ushahidi wake, hivyo kuiomba Mahakama kuridhia leo atoe ushahidi shahidi mmoja tu
Kwa upande wake mshtakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo, alipoulizwa endapo anaridhia maombi hayo alihoji kwanini Jamhuri haikujiandaa na mashahidi angalau watatu (3) kama ambavyo Mahakama ilielekeza huko nyuma ili pale inapotokea mmoja amepata dharura basi angalau wawili (2) watoe ushahidi wao?
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu Renatus Mkude aliieleza Mahakama kuwa shahidi wa pili (Askari mpelelezi) aliyekusudiwa kutoa ushahidi wake leo ambaye amepata dharura wanaamini angetumia muda mrefu pengine hata zaidi ya siku moja ndio maana hawakumuandaa shahidi mwingine watatu (3), hoja hiyo ilikubaliwa na pande zote na Mahakama ikaendelea na ratiba yake ya siku,
Wakili wa Serikali Mkuu Renatus Mkude alianza kwa kuitaarifu Mahakama kuwa shahidi wa leo ambaye kimsingi ni shahidi wa 11 wa Jamhuri ni wa kificho, na kwamba shahidi huyo anatambulika kama ‘P7′
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Thawabu Issa, P7 ameiambia Mahakama kuwa ana miaka 26, Dini yake ni Mkiristo, na kwamba yeye anajishughulisha na uendeshaji wa Bajaji, akifanyia kazi zake kwenye eneo la Kwa Morombo, Arusha, tena akiwa na uzoefu wa kufanya kazi hiyo kuanzia mwaka 2023
Amesema eneo hilo la Kwa Morombo kuna watu wengi wanaojishugjulisha na shughuli mbalimbali kama vile Madereva Bajaji, Mama N’tilie, lakini pia lipo Duka linalouza mahitaji mbalimbali ya nyumbani
Katika maelezo yake, P7 anasema mnamo Tarehe 03/04/2025 majira ya jioni, alikuwa kijiweni hapo wanapopaki Bajaji, ambapo wakiwa kwenye mazungumzo yao ya kawaida ghafla mtu mmoja akaibua mazungumzo mengine tofauti na yale ya mwanzo akawauliza wenzake endapo wamesikia kwamba CHADEMA wamesema watazuia uchaguzi wa mwaka huu (2025)?
Shahidi akaendelea kueleza kwamba, mtu huyo aliyeibua hoja ya CHADEMA kuzuia uchaguzi akawa anendelea kuwasimilia wenzake kuwa CHADEMA wamesema watakinukisha mbaya, pia wamesema kwamba Polisi wanaiba kura, na kwamba hata ukienda Mahakamani hautopata haki kwa sababu Majaji ni vibaraka wa CCM, na kwamba mwaka 2024 (wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa) Tume ya Uchaguzi ilipewa maelekezo ya kukata wagombea wa CHADEMA
Shahidi huyo wa siri ‘P7’ anasema wakiwa wanaendelea kubishana yeye alihamasika kupitia yale maneno, na kwamba baada ya kusikia hayo maneno ikabidi aingie kwenye mtandao wa kijamii wa Youtube ya Jambo TV, huku akiwa anatumia simu yake ya kiganjani (simu janja) akakuta video ya Lissu akizungumza maneno hayo yaliyokuwa yanajadiliwa kijiweni
Anasema wakiwa wanaendelea na mjadala wao, baada ya dakika chache kuna watu walikuja na kuwaambia wapo chini ya ulinzi, na kwamba watu hao wakajitambilisha kuwa wao ni askari,
Anaeleza baada ya watu hao ambao ni askari kufika wengine walikimbia lakini yeye na mwenzake P4 wakakamatwa, na baada ya hapo wakapelekwa kwenye Kituo cha Polisi Muriet, ambapo baada ya kufika kituoni hapo wakakaa kama dakika 45 kisha wakachukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi Central mjini (Arusha), na hapo wakaingizwa ofisi ya RCO
Anaeleza kuwa wakiwa Ofisini kwa RCO Arusha pale Center Police waliambiwa wanashtakiwa kwa kosa la kufanya fujo, baadye akaandika maelezo na kupelekwa mahabusu kabla ya asubuhi ya siku iliyofuata kufuatwa na ndugu zake, akadhaminiwa na kupewa ratiba ya kwenda kuripoti kituo cha polisi

P7 alirudi tena Polisi tarehe 17/04/2025 ambapo baada ya kufika aliambiwa ataandiaka maelezo yake upya, akaandika maelezo kama aliyoyatoa Mahakamani leo, na huo ndo ukawa mwisho wa ushahidi wake;
Baada ya hapo ilikuwa nafasi ya Mahakama kumpatia nafasi mshtakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo kuanza kumuuliza shahidi huyo ‘P7’ maswali ya dodoso (cross examination)
Katika maswali hayo ya dodoso, Lissu alianza kwa kueleza namna anavyofahamu eneo analotokea shahidi huku akimsisitiza kujibu maswali kama ambavyo ataulizwa:-
Lissu: Ujibu maswali bila hofu
Shahidi: Hata hivyo sikuogopi
Lissu: Uliandika maelezo Polisi mara ya wa kwanza tarehe 03/04/2025 na mara ya pili tarehe 17/04/2025 ni sawasawa?
Shahidi: Sahihi kabisa
Lissu: Maelezo ya kwanza uliyoandika ya tarehe 03/04/2025 yalihusu tuhuma ya wewe kufanya kosa na kutaka kufanya fujo, kweli si kweli?
Shahidi: Kweli
Lissu: Hayo maeelezo uliyoandika ya kosa hilo yako wapi?
Shahidi: Sijui, ila nakumbuka maelezo ya tarehe 03/04/2025 ndio hayo hayo niliyoandika tarehe 17/04/2025
Lissu: Tarehe 03/04/2025 uliandika maelezo au hukuandika?
Shahidi: Waliniandika
Lissu: Hayo maelezo yako wapi?
Shahidi: Sikumuomba askari, niliandikwa na kuondoka
Lissu: Vilevile uliandika maelezo tarehe 07/04/2025, kweli si kweli?
Shahidi: Kweli
Lissu: Ukionyeshwa hayo maelezo utayatambua?
Shahidi: Ndio, nitayatambua
Lissu: Majaji naomba shahdii aonyeshwe maelezo yake..

Hapa upande wa Mashtaka (Jamhuri) kupitia Wakili Thawabu Issa ukakabidhi maelezo hayo kwa karani kisha askari akamkabidhi shahidi P7, Lissu akamtaka shahidi kuangalia maelezo hayo na kujithibitishia kama ndio maelezo aliyoaandika tarehe 17/04/2025,
Shahidi alithibitisha kuwa ndiyo maelezo aliyoandika na kuanza kusomewa na Lissu maelezo hayo ambapo alikubali yapokelewe na Mahakama kama kielelezo, Mahakama ilipokea maelezo hayo na kuyapa jina la kielelezo D10, kisha Lissu akaendelea kuhoji, Shahidi umewaeleza Majaji kama pale Kwa Mromboo kuna watu wengi, kweli si kweli?
Lissu: Waeleze Majaji kama katika hicho kielelezo ulichonacho mkononi kina hayo maelezo
Shahidi: Hayapo
Lissu: Umeeleza kwenye ushahidi wako ukiwa Kwa Mromboo mlikuwa mnazungumza mazungumzo ya kawaida kijiweni, kweli si kweli?
Shahidi: Kweli
Lissu: Umeeleza kwamba baada ya hapo kuna mtu akaibua maelezo mengine akisema hamjasikia CHADEMA watazuia uchaguzi wa mwaka huu, kweli au si kweli
Shahidi:Kweli
Lissu: Waeleze Majaji kama hayo maneno yapi kwenye maelezo ya karatasi yako?
Shahidi: Ndio
Lissu: Nionyeshe yako wapi?
Shahidi: Nimesema kwamba ‘alianzisha lakini…’
Lissu: Umeandika hivi tukiwa kijiweni kwetu pale Kwa Mromboo ilianzishwa mada ingawa alieanzisha mada nadhani ilikua inazungumzia kauli za Lissu, hayo maneno ya kuzuia uchaguzi yapo kwenye maelezo yako?
Shahidi: Hapana
Lissu: Umesema kwamba huyo mtu mmoja muanzisha mada akasema ‘tena wamesema watakinukisha mbaya, kweli si kweli?
Shahidi: Kweli
Lissu: Waeleze Majaji kama hayo maneno yapo kwenye maelezo yako?
Shahidi: Yapo
Lissu: Yako wapi?
Shahidi: Watakinukisha
Lissu: Swali langu je, kuna mahali umeandika kuwa hayo maneno yalisemwa na mtu mmoja?
Shahidi: Hapana
Lissu: Shahidi umesema hivi, huyo mtu mmoja akasema Polisi wanaiba kura hata ukienda Mahakamani hautopata haki kwa sababu Majaji ni vibaraka wa CCM, kweli si kweli?
Shahidi: Kweli
Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kama kuna maneno kwamba ‘Majaj hawatendi haki kwa sababu ni vibaraka wa CCM’
Shahidi: Ulisema Majaji hawatendi haki
Lissu: Hayo maneno vibaraka wa CCM yapo au hayapo?
Shahidi: Hayapo
Lissu: Waeleze Majaji kama kwenye hayo maelezo yako umetaja Tume ya Uchaguzi
Shahidi: Hayapo
Lissu: Waeleze Majaji kama kwenye maelezo yako umetaja habari ya Uchaguzi wa 2024 hata mara moja
Shahidi: Hakuna
Lissu: Ulisahau ulichokua unaandika Polisi?
Shahidi: Nilikuwa naandika maelezo sio kitabu
Lissu: Umesema wakati mnabishana ulipata hamasa kutokana na hayo maneno
Shahidi: Kweli
Lissu: Waleze waheshimiwa Majaji kama hayo maneno yapo katika maelezo uliyokuwa unatoa Polisi
Shahidi: Hapana
Lissu: Kwenye ushahidi wako umesema kwamba baada ya kusikia maneno ikabidi uingia mtandao wa YouTube kwa kutumia simu yako janja
Shahidi: Kweli
Lissu: Wale Majaji kwenye maelezo yako kama kuna sehemu uliingia YouTube kwa simu yako janja
Shahidi: Nimesema niliingia kwa kutumia.., mi nahisi kuingia mtandaoni lazima uwe na simu
Lissu: Sio lazima unaweza ukatumia kompyuta, tablet unaweza ukatumia hata Televisheni nk
Shahidi: nilitumia simu ndio kitu nilichonacho
Lissu: Waeleze Majaji kama umetaja simu
Shahidi: Sijataja
Lissu: Umesema uliingia kwenye akaunti ya Jambo TV
Shahidi: kweli
Lissu: Waeleze Majaji kama kuna sehemu umeandika uliingia kwenye mtandao wa YouTube wa Jambo TV
Shahidi: hamna
Lissu: Ahsante, waeleze Majaji kama katika maelezo yako uliyonayo kuna sehemu umesema Ulishtakiwa kwa kosa la kutaka kufanya fujo
Shahidi: Rudia swali
Lissu: Nalirudia kaka ili nisiendelee kukaa gerezani (Lissu akarudia swali)
Shahidi: hayo maelezo hayapo
Lissu: Umesema uliandika maelezo na kulala Polisi hadi asubuhi ulipofuatwa na ndugu zako na kupewa dhamana
Shahidi: No nilikuwa naomba kurudia
Lissu: Jibu swali kwanza
Shahidi: kweli
Lissu: Waeleze Majaji kwamba hayo maneno yapo kwenye karatasi yako ya maelezo?
Shahidi: Hayapo
Lissu: Badala yake ulisema ulidhaminiwa lini uliandika kesho yake mchana nilidhaminiwa
Shahidi: Ndio
Lissu: Waeleze Majaji kama kwenye hayo maelezo umetaja mtandao yalipokuwa hayo.maneno.(kukinukisha)
Shahidi: Ndio nilitaja
Lissu: Uko wapi?
Shahidi: Mtandao wa YouTube
Lissu: Akaunti ya nani mtandao wa Youtube
Shahidi: Sijataja
Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kama katika maelezo yako yote umetaja akaunti ya mtandao wowote
Shahidi:…
Lissu: waeleze Majaji kama vijana kuunga mkono kauli za Tundu Lissu ni kosa la jinai
Shahidi: mimi sijui kwa maana mimi si Mwanasheria
Lissu: Waeleze Majaji kama ni makosa kumuunga mkono Tundu Lissu na chama chake
Shahidi: Mimi sijui
Lissu: Mlikuwa mnasisitizana kuzuia uchaguzi kuniunga mkono
Shahidi: Kweli
Lissu: Waeleze Majaji kama kutaka kuuzia uchaguzi ni kosa
Shahidi: Ni kosa ndio maana nikakamatwa
Lissu: Waeleze Majaji kama ulipelekwa Mahakamani
Shahidi: Sijapelekwa
Lissu: Waeleze Majaji kama baada ya tarehe 03/04/2026 hao mapolisi walihangaika na wewe tena
Shahidi: Ndio, maana waliniambia nikaripoti
Lissu: walikuwa wanakuambia nini?
Shahidi: Nafagia nje, nasaini kisha naondoka
Lissu: Hapa umefika kwa sababu ya kosa langu mimi sio lako wewe,
Shahidi: Kwa sababu we ndo umenisababisihia
Lissu: Polisi walikuambia kwa nini wakati unaandika maelezo tena?
Shahidi: Hawakuniambia chochote
Lissu: Waeleze Majaji umekujaje Mahakamani leo
Shahidi: Kwa miguu
Lissu: Kutoka Kilangi, Arumeru?
Shahidi: Nimepanda basi
Lissu: Nani amekuambia uje?
Shahidi: nilienda Polisi
Lissu: Nani aliyekupa nauli ya kupanda basi kuja Dar es Salaam?
Shahidi: Mwanamke wangu
Lissu: Nani anayekuweka mjini hapa?
Shahidi: Si nishakuambia mwanamke wangu
Lissu: Waeleze Majaji kama kuna kiongozi yeyote wa CHADEMA au mwanachama au mfuasi ambaye amekutishia wewe kukudhuru au kutishia maisha yako?
Shahidi: Sijawahi kutishiwa
Lissu: Waeleze Majaji kama kuna kiongozi wa CHADEMA au mwanachama au mfuasi ambae amewahi kutishia kuharibu mali yako?
Shahidi: Huwezi kutishwa kama hujulikani
Lissu: Waeleze Majaji kwamba kama kuna kiongozi yeyote wa CHADEMA au mwanachama au mfuasi amewahi kutishia ndugu yako au rafiki yako kwa sababu ya kutoa ushahidi
Shahidi: Bro maswali yako…
Lissu: Unajua kwa nini umepewa jina la P7?
Shahidi: Kuficha jina langu halisi
Lissu: Kwa nini?
Shahidi: Kwa sababu ya usalama wangu
Lissu: Si umesema hujatishiwa
Shahidi: Ndio sijatishiwa…
Baada ya kuhitimishwa kwa maswali ya dodoso, Jamhuri haikuwa na la ziada, ndipo Majaji wanaosikiliza kesi hiyo wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru wakahairisha hadi kesho, Alhamisi Februari 19.2026, saa 03:00 Asubuhi.