Leo, Oktoba 21, 2025, Tanzania imeungana na mataifa mengine barani Afrika kuadhimisha Siku ya Haki za Binadamu Afrika, siku muhimu inayokumbusha dhamira ya kulinda utu, usawa na haki za binadamu kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.
Katika maadhimisho hayo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimerejea wito wake wa kudumisha misingi ya haki, utawala bora na uhuru wa msingi kwa kila Mtanzania. LHRC imesisitiza umuhimu wa kulinda watetezi wa haki za binadamu na kuhakikisha mazingira salama kwa shughuli zao nchini.
Hata hivyo, taasisi hiyo imeeleza wasiwasi wake kuhusu kuendelea kwa matukio ya ukiukwaji wa haki, ikiwemo vitendo vya utekaji, kupotea kwa watu, na ukosefu wa uwajibikaji wa baadhi ya vyombo vya dola. LHRC imetoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za haraka kukomesha vitendo hivyo na kurejesha imani ya wananchi katika mifumo ya haki na usalama.
LHRC imesisitiza kuwa Watanzania wote wanastahili kuishi katika nchi yenye haki, amani na usawa. Imehitimisha kwa kauli kwamba, “Jamii yenye haki haiwezi kustawi katika mazingira ya hofu; ni jukumu letu sote kulinda utu wa kila mwanadamu.”