Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uhaini inayoendelea kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo dogo ya Dar es Salaam, amelalamikia kitendo cha wanachama na viongozi wa chama anachokiongozwa kuzuiliwa kwenda kumuona gerezani huku akiwa hajaelezwa sababu za msingi za zuio hilo
Akizungumza mbele ya Mahakama, katika kesi hiyo inayosikilizwa mbele ya jopo la Majaji watatu (3) wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru, Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo amedai kuwa mnamo Novemba 12.2025 akiwa gerezani aliitwa na ‘Bwana Jela’ na kuambiwa kuwa ni marufuku kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA kwenda kumtembelea gerezani kuanzia wakati huo, na kwamba alipohoji alijibiwa kuwa hayo ni maelekezo kutoka juu
“Hii ni nchi ya vyama vingi vya siasa, CHADEMA chama ambacho mimi ni Mwenyekiti wake ni chama halali kwa mujibu wa sheria, hivyo si kosa kwa wanachama na viongozi wenzangu kunitembelea gerezani, sasa maafisa wa Magereza ni maafisa wa umma, hivyo hawana mamlaka ya kubagua nani anaruhusiwa kumtembelea mfungwa au mahabusu gerezani na nani haruhusiwi” -Lissu
Tundu Lissu amesema kanuni ya 12 ya kanuni za uendeshaji wa Magereza imeeleza kwa kina kuwa wafungwa wana haki ya kutembelewa sio na ndugu zao, au familia zao tu bali kwa mtu yeyote isipokuwa tu kwa wale waliokatazwa Kwa mujibu wa masharti ya kanuni
Amesema watu waliopigwa marufuku kutembelea wafungwa au mahabusu gerezani ni wale waliowahi kutumikia kifungo gerezani, lakini wengine wote wanaruhusiwa kutembelea wafungwa isipokuwa tu wakati wa mazungumzo yao maafisa wa Magereza wanaruhusiwa kusikiliza mazungumzo hayo ili kujuwa wanachoongea
Aidha, Tundu Lissu amesema tangu alipowekwa mahabusu kwa mara ya kwanza Aprili 10.2025 viongozi na wanachama wa chama hicho wamekuwa wakimtembea gerezani kama kawaida, lakini marufuku hiyo ambayo yeye anadai kuwa ilikuja baada ya kesi yake kuahirishwa Novemba 12.2025.