Latest Posts

MAFUNDI NA WAUNDAJI VIPIMO NCHINI WAASWA KUENDANA NA TEKNOLOJIA

Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma, Bw. Said Ibrahim akizungumza na mafundi na waundaji wa vipimo mbalimbali wakati wa kikao kazi kilichofanyika Februari 18, 2026 Dodoma kwa lengo la kujadiliana masuala muhimu kuhusu sekta hiyo. Meza Kuu (katikati) ni Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi Bw. Francis Olwero

 

Mafundi na waundaji wa vipimo wa Mkoa wa Dodoma wakifuatilia mafunzo ya namna ya kuomba leseni kupitia Mfumo maalumu wa kidijitali wa Wakala wa Vipimo ulioanzishwa hivi karibuni. Mafunzo hayo yalifanyika Februari 18, 2026 wakati wa kikao kazi cha WMA Dodoma na wadau wa vipimo.
Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA), Bw. Francis Olwero akizungumza na mafundi na waundaji wa vipimo mbalimbali wakati wa kikao kazi kilichofanyika baina yao na WMA Mkoa wa Dodoma, Februari 18, 2026 Dodoma kwa lengo la kujadiliana masuala muhimu kuhusu sekta hiyo.

 

 

 

Na WMA – Dodoma

Mafundi wa vipimo, waundaji wa mizani pamoja na wapimaji wa matanki ya kuhifadhia mafuta ardhini wameshauriwa kuelekeza nguvu katika vipimo vya kidijitali kutokana na maendeleo ya teknolojia yanayoleta mabadiliko kila siku.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi, Wakala wa Vipimo (WMA), Francis Olwero, wakati wa kikao kazi na mafunzo kwa kundi hilo, yaliyoandaliwa na Ofisi ya WMA Mkoa wa Dodoma na kufanyika Februari 18, 2026.

Akifungua kikao kazi na mafunzo hayo, Mkurugenzi Olwero aliwaambia washiriki kuwa kukua kwa teknolojia kunailazimu sekta ya vipimo kuendana na mabadiliko yanayotokea ili kazi ziendelee kufanyika kwa tija.

“Mathalani, mifumo ya zamani ya kuomba leseni imebadilika, kwahiyo nanyi muwe tayari kubadilika. Sasa hivi mambo mengi ni ya ki-elektroniki, usikubali kubaki nyuma,” alisisitiza.

Akichanganua zaidi, Mkurugenzi Olwero alitahadharisha kuwa kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia, katika kipindi cha miaka michache ijayo, vipimo visivyo vya ki-elekroniki ikiwemo mizani vitakuwa havitumiki tena hivyo akawashauri mafundi na waundaji wa vipimo hivyo kuhakikisha wanatumia muda huu kujifunza na kuwekeza kwenye vile vya ki-elekroniki ili kuendana na soko.

“Jaribuni kujifunza kutengeneza mizani za ki-elektroniki. Muda siyo mrefu mtaona hizi za kawaida hazitumiki tena. Kwahiyo, wewe kama unataka kufanya kazi ya ufundi wa mizani kwa miaka kama mitano ijayo, uwe umeshabobea kwenye elektroniki.”

Katika hatua nyingine, aliwashauri mafundi na waundaji wa vipimo kufanya kazi kwa ushirikiano baina yao lakini pia kutoa ushirikiano kwa Maafisa wa WMA walioko katika maeneo yao ili kuhakikisha kazi inafanyika kwa mujibu wa sheria na kila kundi linanufaika ipasavyo.

Akifafanua, aliwataka kujitambulisha kwa Meneja wa WMA wa eneo husika pindi wanapoenda kufanya kazi ili uwepo wao katika eneo hilo utambuliwe.

“Itamsaidia Meneja kuthibitisha kama leseni yako ni halali ili yeye pia aweze kukusaidia endapo utapata changamoto ya kikazi. Hiyo itakusaidia wewe pia kufanya kazi yako kwa ujasiri na kujiamini,” alisisitiza Mkurugenzi.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Umoja wa Mafundi Mizani Dodoma, Shaidu Rwemuka alipongeza jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na WMA Mkoa wa Dodoma kwa kuandaa vikao kazi vya mara kwa mara akisema vinasaidia kuwajengea uelewa zaidi na kuwawezesha kufanya kazi yao kwa ufanisi na nidhamu.

Aidha, kuhusu kuanzishwa kwa Mfumo huo mpya wa kielektroniki, Rwemuka alisema kuwa kumesaidia mambo mengi ikiwemo kuokoa muda.

“Awali, ilikuwa ukusanye taarifa, uende sehemu mbalimbali ikiwemo WMA na BRELA na baada ya mchakato kukamilika tulitakiwa kufuata leseni zetu kwa Meneja wa WMA wa Mkoa. Kwa sasa unaipata leseni yako kutoka kwenye Mfumo ukiwa popote na wakati wowote.”

Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma, Bw. Ibrahim Said ambaye aliratibu kikao kazi na mafunzo hayo, alibainisha kuwa Ofisi yake imekuwa ikiandaa kikao kazi na wadau hao wa vipimo kila baada ya miezi mitatu kwa lengo la kukumbushana majukumu ya kazi pamoja na kutatua changamoto ambazo hukutana nazo wakati wa kutekeleza majukumu ya kila siku.

“Miongoni mwa changamoto iliyokuwa inatukabili kwa sasa ni uelewa wa kutumia Mfumo mpya wa kujisajili ambao Wakala tumeuanzisha hivi karibuni ambapo mafundi wetu wote wanatakiwa kuutumia kuweka taarifa zao kwa ajili ya maombi ya leseni kwa shughuli wanazofanya,” alieleza.

Alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo, Ofisi yake iliona ni vema kikao kazi hicho kikaambatana na mafunzo ya namna ya kutumia Mfumo huo.

Mfumo huo mpya wa kujisajili mafundi na waundaji vipimo nchini unatambulika kama OSA (Online Service Application) na unapatikana kupitia kiungo osa.wma.go.tz ukiwa ni sehemu ya Mfumo Mama wa WMA uitwao WMA-MIS.

Wakala wa Vipimo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia sekta ya vipimo nchini ikiwemo usajili na utoaji leseni kwa mafundi na waundaji wa vipimo vya aina mbalimbali nchini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!