Mahakama ya Afrika Kusini imeingilia kati na kusitisha mpango wa kufanyika kwa mazishi ya faragha ya Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, yaliyopangwa kufanyika nchini humo, hatua iliyochochewa na mvutano kati ya familia ya marehemu na Serikali ya Zambia.
Taarifa ya kusitishwa kwa mazishi hayo imetolewa kwa waombolezaji waliokuwa tayari wamekusanyika baada ya misa maalum ya kumwombea marehemu kukamilika, na kusababisha mshituko na sintofahamu kubwa.
Serikali ya Zambia iliwasilisha kesi ya dharura katika Mahakama Kuu ya Pretoria, ikiomba kusimamishwa kwa mazishi hayo yaliyokuwa yamepangwa na familia ya Lungu, ikisisitiza kuwa kama rais wa zamani, marehemu anastahili kupewa heshima ya kuzikwa nyumbani Zambia kwa mujibu wa utaratibu wa kitaifa.
Mahakama imesema mazishi hayawezi kuendelea kufuatia makubaliano kati ya wahusika waliokuwa wamewasilishwa mbele ya jopo la mahakama, lakini imeelezwa kuwa mazishi yoyote hayataweza kufanyika hadi mapema mwezi Agosti.
Mzozo huu ni sehemu ya mvutano wa muda mrefu kati ya Lungu na mrithi wake, Rais Hakainde Hichilema, ambapo familia ya Lungu imekuwa ikisisitiza kuwa Rais Hichilema hapaswi kuhudhuria mazishi hayo, kutokana na tofauti za kisiasa na madai ya kutotendewa haki wakati wa uhai wake.
Baada ya Lungu kufariki dunia akiwa Afrika Kusini akiwa na umri wa miaka 68, familia yake ilitaka kushughulikia taratibu zote za mazishi, ikiwa ni pamoja na kuusafirisha mwili wake, huku Serikali ya Zambia ikitaka kudhibiti mchakato huo kama sehemu ya heshima ya kitaifa.
Hadi sasa, haijafahamika wazi ni lini na wapi maziko hayo yatafanyika rasmi, huku vyanzo vya karibu na familia ya marehemu vikieleza kuwa mazungumzo mapya yanaendelea kufanyika ili kufikia muafaka wa mwisho.