
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi kwani ndiyo tunu msingi ya Taifa.
Malima ameyasema hayo Novemba 4, 2025, ofisini kwake, wakati alipokutana na Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Morogoro, Dkt. George A. Pindua, ambaye alifika kujadili maandalizi ya hafla yake ya kuingizwa kazini iliyokuwa imepangwa kufanyika Novemba 9, 2025.
Mkuu wa Mkoa pia amewashukuru wananchi wa Morogoro kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, ambao uliwawezesha Mkoa huo kuwa tulivu na kisha kurejea katika shughuli zao za kila siku kwa amani.
Sambamba na hilo amempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kwa uongozi wake thabiti katika kudumisha usalama na amani hapa nchini.
“Matokeo ya hali ya utulivu na usalama katika Mkoa wa Morogoro yamepatikana kwa kushirikiana kwa wadau wote wa Mkoa huu. Ushirikiano huu umekuwa mfano bora kwa mikoa mingine,” amesema Malima.
Kwa niaba ya viongozi wa dini, Askofu Mteule Dkt. Pindua amempongeza Malima kwa ushirikiano aliouonesha tangu aanze kuongoza Mkoa wa Morogoro, lakini zaidi katika kipindi hiki cha maandalizi ya uchaguzi ambapo amewashirikisha viongozi wa dini katika vikao mbalimbali vya kuimarisha amani na utulivu Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa nae amewashukuru viongozi wote wa dini, wazee, vijana, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji, wanahabari, mama lishe, baba lishe, wamachinga, machifu, madereva wa mabasi na bodaboda, pamoja na asasi zisizo za kiserikali kwa mchango wao mkubwa katika kuhimizia wananchi kushiriki uchaguzi Mkuu kwa amani.
Shukrani hizo pia amezielekeza kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Vijiji/Mitaa pamoja na watumishi wote wa umma na taasisi za serikali kwa kazi kubwa ya kuhakikisha amani inadumu ndani ya Mkoa wa Morogoro.
Kwa upande mwingine, Malima na Askofu Mteule Dkt. Pindua walijadili kuahirishwa kwa ibada ya kuingizwa kazini kwa Askofu huyo Mteule pamoja na Msaidizi wake Mch. Peter Michael Makalla, ambayo awali ilipangwa kufanyika Novemba 9, 2025 ambayo sasa imepangwa kufanyika Desemba 14, 2025.