Latest Posts

MAMIA WACHANGAMKIA FURSA YA KUPAMBANA NA FOLENI MIJINI, ZAWADI YAONGEZWA

Mamia ya wanafunzi wa taaluma za uhandisi wamejitokeza kushindana katika changamoto ya ubunifu wa kuondoa kero za foleni mijini iliyoanzishwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Ulega alisema hadi kufikia siku ya mwisho ya wanafunzi hao kuwasilisha maandishi yao ya kitaaluma ya kupunguza foleni, maandiko 561 yamepokewa.

Waziri huyo alisema kwa ujumla, wizara na taasisi zilizo chini yake, zimetiwa moyo sana na mwitikio wa wanataluma na jamii ya Watanzania kwa ujumla, kwani imeonyesha kiu ya dhati ya kukabiliana na changamoto zilizopo kwa kutumia utaalamu wa nyumbani.

“Kusema kweli hatukutarajia kupata maombi mengi kiasi hiki. Katika hayo 561, kuna maandiko mengine hatujayatumia kwa sababu yalifikishwa kwetu nje ya muda na mengine na watu wasio wanafunzi. Kama kusingekuwa na vigezo, idadi ingekuwa kubwa zaidi. Lengo letu la kutaka wanafunzi wa taaluma za uhandisi wachemshe bongo zao na kukuna vichwa hasa kutafuta suluhu za kero zinazoikumba jamii yetu limefanikiwa kwa asilimia 100. Huu ni mwanzo mzuri na tutaendelea kutoa chemsha bongo za namna hii kwa kadri hali itakavyoruhusu,” alisema.

Shindano hilo la ubunifu lilitangazwa na Waziri Ulega kwa mara ya kwanza Februari 23 mwaka 2026 wakati alipokuwa akizungumza na jumuiya ya wanafunzi wa taaluma za uhandisi katika ukumbi wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Katika maelezo yake, Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, alisema shindano hilo litahusu wanafunzi wa taaluma za Uhandisi (Engineering), Ukadiriaji Majenzi (Quantity Surveyors), na Ubunifu Majengo (Architects).

Katika hatua nyingine, Ulega jana alitangaza kwamba kutokana na mwamko mkubwa uliooneshwa, zawadi kwa washindi sasa zimeongezwa kutoka katika kiwango cha awali cha shilingi milioni 10 zilizotakiwa kugawanywa kwa washindi watatu wa kwanza.

Mshindi wa kwanza atapata zawadi ya shilingi milioni 10, wa pili atapata milioni tano, wa tatu shilingi milioni tatu, wa nne shilingi milioni mbili, wa tano shilingi milioni moja huku kuanzia mshindi wa sita wa kumi wakipata shilingi laki tano kila mmoja.

“Pamoja na zawadi hizo za fedha taslimu, washindi wote watapewa zawadi ya kompyuta mpakato yaani laptop na pia kutafutiwa mahali pa kwenda kufanya mafunzo kazini (field) huku baadaye akipewa nafasi ya kuonyesha namna wazo lake litakavyofanya kazi,” alisema Ulega.

Pia, Ulega alitangaza jopo la wataalamu litakalofanyia kazi mawasilisho hayo ya wasomi ambapo mshindi anatarajiwa kutangazwa mwishoni mwa mwezi huu.

Baadhi ya wajumbe wa jopo hilo ni mbunifu na mchoraji maarufu nchini, Masoud Kipanya, ambaye mara nyingi amekuwa akitoa maoni yake binafsi kupitia vipindi vya redio kuhusu namna ya kupunguza foleni mijini.

Wajumbe wengine wa jopo hilo ni Mhandisi Gaspar Marco kutoka Wakala wa Babarara Tanzania (TANROADS) ambaye ndiye atakuwa Mwenyekiti wa jopo hilo. Wajumbe wengine na taasisi wanazotoka kwenye mabano ni Deusdedit Karugendo (CRB), Khadija Salum (TBA), Ramadhani Maziku (AQRB) na Joseph Soka kutoka Chama cha Wahandisi Tanzania.

Wajumbe wengine ni wahadhiri kutoka katika vyuo vikuu tofauti nchini ambao ni Dkt. Jaqueline Masaki (UDSM), Dkt. Lupakisyo G. Mwalwiba (MUST -Mbeya) na Dkt. Ramadhani Marijani (UDOM).

Wengine ni ACP. Joseph Mwakabonga- Kamishna Msaidizi wa Polisi-Usalama Barabarani, Phares Ngeleja kutoka TARURA, Salum Hamza kutoka Chama cha Madereva Daladala jijini Dar es Salaam na Mhandisi Erick Nestory ambaye ni Katibu wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB).

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!