Baraza la Madiwani la Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara limeidhinisha bajeti ya shilingi bilioni 39.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, huku kipaumbele kikubwa kikiwekwa katika kuboresha miundombinu ya barabara na mifereji ndani ya manispaa hiyo.
Katika kikao cha baraza hilo kilichofanyika leo Machi 5, 2026, madiwani walipitisha mpango wa kutenga shilingi milioni 600 kwa ajili ya ununuzi wa greda jipya litakalosaidia kuchonga na kuboresha barabara za mitaa, hatua inayotarajiwa kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi.

Mbali na ununuzi wa greda hilo, baraza pia limetenga shilingi milioni 155 kwa ajili ya shughuli za kuchonga barabara katika maeneo mbalimbali ya manispaa. Hatua hiyo inalenga kuboresha upatikanaji wa miundombinu bora ya barabara, hasa katika mitaa ambayo imekuwa ikikumbwa na changamoto za usafiri.
Aidha, kiasi kingine cha shilingi milioni 155 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mifereji ya maji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza athari za maji kuingia kwenye makazi ya wananchi hususan wakati wa msimu wa masika.
Baadhi ya madiwani wa manispaa hiyo wameeleza kuridhishwa na maamuzi ya bajeti hiyo, wakisema kuwa uwekezaji katika ununuzi wa greda pamoja na ujenzi wa mifereji ni hatua muhimu itakayochochea maendeleo ya miundombinu na kuboresha maisha ya wananchi wa Mtwara Mikindani.
Wameeleza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo utaongeza ufanisi katika matengenezo ya barabara za mitaa na kupunguza changamoto za mafuriko katika maeneo ya makazi, hivyo kuifanya bajeti hiyo kuwa na umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya manispaa na ustawi wa wananchi wake.
