Marekani imeishutumu Iran kwa kuanzisha mashambulizi ya mtandaoni kwenye kampeni za Urais za Kamala Harris na Donald Trump, na kuwalenga wapiga kura wa Marekani ili kuchochea mifarakano na kudhoofisha imani kwa taasisi za kidemokrasia za nchi hiyo.
Tathmini kutoka Shirika la Upeleleza la Marekani FBI na mashirika yake mengine ya kiusalama inaashiria kuwa ni mara ya kwanza kwa serikali ya Marekani kutoa lawama huku kukiwa na hofu mpya ya tishio la kuingiliwa kwa uchaguzi wa kigeni katika uchaguzi wa nchi hiyo.
Maafisa wa Kampeni ya Trump waliinyooshea kidole Iran tarehe 10 Agosti, 2024 kwa kudukua ujumbe wake wa ndani, hata hivyo maafisa wa Iran walikanusha.
Vyanzo vinavyofahamu uchunguzi huo viliiambia kampuni ya habari mshirika wa BBC wa Marekani, CBS News, kwamba wanashuku kuwa wavamizi wa kitandao wa Iran pia waliilenga kampeni ya mgombea urais wa chama cha Democratic Kamala Harris.
“Tumeona shughuli kali za Iran zinazoongezeka wakati wa mzunguko huu wa uchaguzi, hasa unaohusisha operesheni za ushawishi zinazolenga umma wa Marekani na operesheni za mtandao zinazolenga kampeni za urais,” FBI, Ofisi ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa na Wakala wa Usalama wa Mtandao na Miundombinu, ambayo inawajibika kulinda mifumo ya kompyuta ya serikali ya Marekani ilieleza katika taarifa siku ya Jumatatu.
Kampuni ya mtandao wa Google imeeleza kuwa mwezi huu wadukuzi wanaoungwa mkono na Iran walikuwa wakilenga kampeni za urais wa Democratic na Republican.
Kikundi cha wadukuzi kinachojulikana kama APT42 chenye uhusiano na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kilikuwa kikiwafuatilia watu mashuhuri na mashirika nchini Israel na Marekani wakiwemo maafisa wa serikali na kampeni za kisiasa, Google ilisema katika ripoti yake