Watanzania wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kulinda na kudumisha amani ya Tanzania kwa ustawi na maendeleo binafsi na ya Taifa, Wito ukitolewa kwa jamii hususani Vijana kuwekeza katika ujuzi ili kuwawezesha kujikita katika shughuli za kiuchumi na uzalishaji mali ili kujiingizia kipato na kujiletea maendeleo yao binafsi na ya Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa wakati huu ambapo Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetangaza na kuanza uwekezaji mkubwa wa kuwezesha wananchi kiuchumi hususan Vijana, kwa kutoa mabilioni ya fedha kupitia wizara mbalimbali ikiwemo ahadi ya utoaji wa Shilingi Bilioni 200 za Mikopo kwa makundi ya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo, Bilioni 2 za watengeneza maudhui mtandaoni, mikopo ya Halmashauri pamoja na kuundwa kwa Wizara maalumu ya maendeleo ya Vijana iliyojikita katika kusimamia fursa za Vijana na kutatua changamoto zilizopo.
“Amani ni muhimu kwasababu bila amani huwezi kufanya chochote na amani huvunjika pale ambapo tunakuwa na Vijana wasiokuwa na ajira ama ujuzi wowote ule ni lazima ataenda ndivyo sivyo na kuvunja amani aidha kwa kuiba ama kushiriki katika matukio mengine ya uvunjifu wa amani.” Amesema Bw. Dickson Mazengo, Mkazi wa Ubungo, Dar Es Salaam.
Akieleza zaidi kuhusu umuhimu wa kulinda amani, Bw. Mazengo amesisitiza umuhimu pia wa kushirikisha ujuzi mbalimbali kwa watu wengine kwenye jamii, akisema kupitia hilo anaamini kuwa kila mmoja atapata shughuli ya kufanya na hivyo kunufaisha mnyororo mzima unaomtegemea na kutengeneza utulivu wa jamii unaozalisha amani kwenye Taifa.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa amani inatajwa kama zaidi ya kutokuwepo fujo, ikielezwa kuwa ni utaratibu wa kihamii unaojengwa juu ya msamaha na ushirikiano na kusisitiza jukumu la kila mwananchi kuwa balozi wa amani kuanzia ngazi ya familia, jamii na Taifa ili kuunda ulimwengu bora kwa kila mmoja kwani amani husaidia katika maboresho ya huduma na ujenzi wa miundombinu msingi ya kijamii na kiuchumi kwa kila mmoja.