Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, amewahakikishia Watanzania kuwa nchi imebaki salama na yenye umoja katika kipindi cha siku 100 tangu kuhitimishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ambao ulimshuhudia Samia Suluhu Hassan kama mshindi wa Urais.
Akizungumza na BBC Swahili leo, Februari 10, 2026, Msigwa amesema kuwa licha ya changamoto na ghasia zilizojitokeza baada ya uchaguzi, serikali imefanikiwa kurejesha utulivu na kuendelea na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
“Kwa ujumla taifa liko salama katika siku hizi 100, kwa mara nyingine Tanzania imeonesha namna ambavyo inaweza kuhakikisha nchi iko salama, watu wake wako salama na wanaendelea na shughuli zao kama kawaida. Kwasababu kwetu hili ndio jambo la muhimu kuliko yote kwamba baada ya uchaguzi pamoja na changamoto zilizojitokeza lakini hivi navyozungumza Watanzania ni wamoja”, ameeleza.
Msigwa amebainisha kuwa shughuli za kiuchumi zinaendelea kama kawaida kote nchini, huku serikali ikijikita katika kutekeleza majukumu ya kibajeti kama ilivyopangwa. Ameeleza kuwa jambo la muhimu zaidi kwa serikali ni kuhakikisha amani inadumu ili kuruhusu wananchi kuendelea na maisha yao bila hofu.
Aidha, Msigwa amegusia kazi inayofanywa na Tume ya Uchunguzi inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, iliyoundwa kuchunguza vifo na majeraha na matukio mengine yaliyotokana na maandamano yaliyotokea kipindi cha uchaguzi. Amesema Tume hiyo inafanya kazi kwa uwazi na uhuru mkubwa, tofauti na hofu iliyokuwepo awali wakati inatangazwa.
Msigwa amesisitiza kuwa serikali itafanyia kazi mapendekezo yatakayotolewa na ripoti ya Jaji Chande mara itakapokamilika. Amesema ni mapema mno kuanza kuhukumu au kutoa maamuzi kabla ya ukweli wa kisayansi na kisheria kubainishwa na tume hiyo.