Wadau wa maendeleo wa Jimbo la Mtwara Mjini wametoa mapendekezo mbalimbali kwa Mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Arthur Nanauka, wakimtaka kuyapa kipaumbele masuala yatakayorahisisha huduma kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

Mapendekezo hayo yametolewa Februari 17,2026 katika kikao kilichowakutanisha viongozi na wadau wa maendeleo wa jimbo hilo, ambapo pamoja na mambo mengine walisisitiza umuhimu wa kuanzisha vituo vya kujazia gesi ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kwa urahisi zaidi.

Aidha, wadau hao wameeleza haja ya kufanyia marekebisho Kivuko cha Kirambo kwa lengo la kuboresha usafiri na kurahisisha shughuli za kila siku za wananchi, hatua itakayosaidia pia kukuza shughuli za kiuchumi katika maeneo husika.
Kwa upande wake, Dkt. Nanauka amesisitiza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake ataendelea kujikita katika kukuza uchumi wa wananchi pamoja na kuboresha miundombinu ya Jimbo la Mtwara Mjini na kueleza kuwa kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi ni miongoni mwa vipaumbele vyake ili kuongeza ushiriki wao katika maendeleo.
Katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mheshimiwa Abdallah Mwaipaya, amewahimiza wananchi kujisajili katika Daftari la Mkazi kupitia viongozi wa maeneo yao, akibainisha kuwa hatua hiyo itaimarisha ulinzi na usalama kwa kutambua wageni wanaoingia katika maeneo yao.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara aliwataka wananchi kutumia vyema fursa za uwekezaji zinazozidi kujitokeza mkoani humo, akieleza kuwa Mkoa wa Mtwara umeanza kuvutia wawekezaji kutokana na fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo.