Na; mwandishi wetu
Jumatatu ya juma lijalo, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam inatarajiwa kutoa maamuzi ya shauri lililofunguliwa Mahakamani hapo na Mwanaharakati Dkt. Willbroad Slaa anayepinga ‘danadana’ za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoko jijini Dar es Salaam za kutopatiwa dhamana kwa muda mrefu
Itakumbukwa kuwa, Dkt. Slaa mwenye umri wa miaka 76 ambaye pia ni Mwambata wa ‘Sauti ya Watanzania’ awali alikamatwa na maafisa wa Jeshi la Polisi nyumbani kwake Tegeta, jijini Dar es Salaam usiku wa Januari 09.2025, na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jioni ya Januari 10.2025 ambapo alisomewa shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa X ambao zamani ulijulikana kama Twitter
Hata hivyo licha ya kusomewa shtaka hilo katika kesi ya jinai namba 993 ya mwaka 2025, shtaka lililosomwa na jopo la Mawakili watatu (3) wa serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Clemence Kato akishirikiana na Tumaini Mafuru na Abdul Bundala, lakini licha ya kwamba kosa hilo linadhaminika Dkt. Slaa ameendelea kusota rumande bila kupatiwa dhamana
Mawakili wa Dkt. Slaa wakiongozwa na Peter Madeleka, Hekima Mwasipu, Mwanaisha Mndeme, Edson Kilatu na wengineo wameeleza kuwa wamefanya jitihada za makusudi kuhakikisha mteja wao anapatiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini wamekuwa wakipigwa ‘danadana’ hadi sasa huku mteja wao akiwa hajasikilizwa hadi sasa, jambo linaloibua maswali inakuwaje mtuhumiwa ambaye hajasikilizwa, kosa lake linadhaminika lakini anazungushwa kupatiwa haki yake ya Kikatiba?, ndipo Mawakili hao kwa niaba ya mteja wao wamefikia maamuzi ya kukimbia Mahakama Kuu
Alhamisi Januari 23.2024 Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam shauri la kupinga ‘danadana’ za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu juu ya dhamana ya Dkt. Slaa limesikilizwa chini ya Jaji Anold Kirekiano
Mabishano ya hoja za kisheria kutoka kwa Mawakili wa pande zote mbili yaani upande wa waleta maombi (Dkt. 7Slaa) na upande wa utetezi (Mawakili wa Serikali kwa niaba ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu) yamechukua takribani saa 4, ambapo upande wa waleta maombi umeileza Mahakama hiyo kuwa hawafurahishwi na namna Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inavyoshughulikia suala hilo, jambo ambalo limepingwa vikali na upande wa utetezi ukieleza kuwa kwa kiasi kikubwa upande wa mtuhumiwa ndio unaokwamisha suala hilo maana mara zote wamekuwa wakileta mapingamizi Mahakamani kila shauri hilo linapotajwa
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam chini ya Jaji Anold Kirekiano anayesikiliza shauri hilo ameahidi kutoa maamuzi ya suala hilo Jumatatu ya juma lijalo saa 04 asubuhi, hivyo mtuhumiwa karejeshwa rumande hadi siku hiyo
Akizungumza na wanahabari nje ya viunga vya Mahakama hiyo, Wakili Peter Madeleka amesema hata hivyo kesho, Ijumaa ya Januari 24.2025 saa 3 asubuhi watarejea tena Mahakamani hapo kwa kuwa mteja wao (Dkt. Slaa) amefungua shauri lingine la kuomba Mahakama Kuu kuifuta kesi ya msingi iliyofunguliwa na Jamhuri/ serikali kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na kile walichodai kuwa kesi hiyo haina mashiko
“Zuio lililowekwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam lilikuwa limekiuka sheria na lina lengo la kuzuia upatikanaji wa haki ya dhamana ya mteja wetu, kimsingi baada ya Mheshimiwa Jaji kutupa nafasi ya kutusikiliza na kuzungumza hoja hizo kwa kirefu, tumenukuu vifungu kadhaa vinavyounga mkono hoja zetu ambazo zinatufanya tuamini kwamba kinachofanyika Kisutu ni kuchelewesha haki ya msingi ya mteja wetu” -Wakili Madeleka
“Ndugu zangu mnapaswa kukumbuka kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 107, A Ibara ndogo ya 2b ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mahakama imepigwa marufuku kuchelewesha haki ya mtu yeyote Mahakamani bila sababu za msingi, sasa danadana ambazo zilikuwa zinafanywa pale Kisutu ndio imetufanya sisi tuje Mahakama Kuu hapa, kwa ajili ya kuiomba Mahakama itumie mamlaka yake ili iweze kutengua mwenendo wote ule na kutamka kwamba ni batili na hivyo kumpa dhamana mteja wetu, kwa sababu dhamana ni haki ya Kikatiba na kisheria” -Wakili Madeleka
Katika shauri la msingi lililofunguliwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dkt. Willbroad Slaa ambaye pia amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden Anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandao namba 14 ya mwaka 2015, ambapo mshtakiwa alisomewa shtaka lake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki, na kwa mujibu wa Wakili Kato alieleza kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 09.2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ikumbukwe kuwa, wakati wote huo ambao mashauri hayo yatakuwa yakiendelea kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, shauri la msingi lililopo kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu litalazimika kusubiri hadi hapo maamuzi ya Mahakama Kuu yatakapotoka.