Latest Posts

MWANAHARAKATI BONIFACE MWANGI ATANGAZA KUGOMBEA URAIS KENYA 2027

Mwanaharakati maarufu wa kijamii nchini Kenya, Boniface Mwangi, ametangaza rasmi kuwania nafasi ya Urais wa nchi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, akieleza kuwa mapambano aliyoyafanya mitaani lazima sasa yaendelee hadi Ikulu.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika Agosti 27, 2025, siku ambayo Kenya huadhimisha Katiba yake, Mwangi alisema harakati zake zitaelekezwa zaidi kwa vijana ambao, kwa mujibu wake, wanahitaji uongozi mpya utakaoleta mageuzi ya kweli ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

“Nimeona kwamba ni lazima niendelee na hii vita tuliyokuwa tunapigania barabarani niipeleke Ikulu. Serikali ya sasa haiwahudumii wananchi, inatuibia na kutuua. Vijana wengi wanasema wanataka uongozi mpya, na mimi nimejitolea kuendesha Kenya mbele,” alisema Mwangi.

Mwanaharakati huyo, ambaye pia aliwahi kukamatwa nchini Tanzania alipohudhuria kesi ya uhaini ya Kiongozi wa Upinzani Tundu Lissu, amesisitiza kuwa kipaumbele chake ni utekelezaji wa Katiba ya Kenya, akidai imepuuzwa na serikali zilizopita. Ameongeza kuwa utekelezaji wake utawezesha kila Mkenya kupata huduma muhimu na maisha bora, sambamba na mapambano dhidi ya ufisadi.

Kwa sasa, Mwangi amejiunga na orodha ya viongozi na wanasiasa waliotangaza nia ya kumng’oa madarakani Rais William Ruto, akiwemo aliyewahi kuwa Jaji Mkuu David Maraga na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i, miongoni mwa wengine.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!