Latest Posts

MZEE WA MIAKA 81 DHIDI YA KIJANA WA MIAKA 43: HATMA YA UGANDA KUAMULIWA LEO KWENYE SANDUKU LA KURA.

Raia wa Uganda leo, Januari 15, 2026, wameminika katika vituo vya kupigia kura kumchagua Rais na Wabunge, huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa katika mitaa ya miji mikuu na maeneo ya vijijini.

Uchaguzi huu unamweka Rais Yoweri Museveni (81), ambaye amekuwa madarakani kwa miongo minne, dhidi ya wagombea wengine saba, akiwemo mpinzani wake mkuu, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine (43). Wakati Museveni anawania muhula wa saba akitegemea uzoefu wake na udhibiti wa vyombo vya dola, Bobi Wine anapeperusha bendera ya mabadiliko akitegemea uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana wanaounda idadi kubwa ya wapiga kura.

Zoezi hili la upigaji kura linafanyika katika mazingira ya wasiwasi kutokana na hatua ya serikali kuminya huduma za intaneti, hali inayotajwa na wapinzani kama mbinu ya kuzuia mawasiliano na uratibu wa kulinda kura. Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa moja asubuhi na vinatarajiwa kufungwa saa kumi alasiri kwa saa za eneo hilo.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, mshindi wa kiti cha urais anatarajiwa kutangazwa rasmi ifikapo Jumamosi mchana, Januari 17, 2026. Dunia nzima inaelekeza macho yake nchini Uganda kuona ikiwa taifa hilo litaingia katika awamu mpya ya uongozi au litaendelea na utawala wa Museveni uliodumu tangu mwaka 1986.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!