Namibia imepanga kuwaua wanyamapori 723 kwa lengo la kutumika kama chakula cha wananchi walioathirika na ukame mkali zaidi wa miaka 100.
Katika taarifa iliyotolewa tarehe 26 Agosti na Wizara ya Mazingira, Misitu na Utalii ya Namibia, ilielezwa kuwa idadi hiyo itajumuisha vifaru, nyati, swala, tembo na pundamilia miongoni mwa wanyama wengine.
Kulingana na Citizen Digital, wizara hiyo ilisema kwamba wanyama hao watapatikana kutoka kwenye hifadhi za taifa na maeneo ya kijamii yenye idadi endelevu ya wanyama.
Kupunguza idadi ya wanyamapori kwa mujibu wa Wizara, kutaweza kupunguza madhara ya ukame kwenye uhifadhi wa wanyamapori kwa kupunguza shinikizo la malisho na upatikanaji wa maji.
“Tunaona hii kama hatua muhimu na inatokana na wajibu wetu wa kikatiba wa kutumia rasilimali zetu kwa manufaa ya wananchi wa Namibia,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza,
“Mbali na hayo, hii ni mfano mzuri wa jinsi uhifadhi wa wanyama pori unavyoweza kuwa na faida. Tunafurahi kwamba tunaweza kutoa msaada kwa nchi yetu wakati huu mgumu.”
Wizara iliongeza kwamba kwa miaka mingi, imekuwa ikitoa nyama kwa ajili ya matukio ya kitaifa, kikanda, na kijadi kulingana na sera na sheria zake.
Namibia ilitangaza hali ya dharura mnamo mwezi Mei kutokana na kuongezeka kwa athari za ukame. Kati ya Aprili na Juni 2024, watu wapatao milioni 1.2 walikabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa chakula na walihitaji hatua za haraka kupunguza pengo la chakula na kulinda maisha yao.
Ukanda wa Kusini mwa Afrika umekuwa ukikabiliwa na ukame mbaya zaidi katika miongo kadhaa huku Umoja wa Mataifa ukiripoti kwamba Namibia ilikuwa imekamilisha asilimia 84 ya akiba yake ya chakula mwezi uliopita.