Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemkabidhi Rais wa Marekani Donald Trump barua rasmi ya uteuzi kwa Tuzo ya Amani ya Nobel, akimsifu kwa juhudi zake katika kutafuta suluhu za migogoro ya Mashariki ya Kati.
Tukio hilo lilijiri Jumatatu, wakati wa mkutano wao Ikulu ya White House, Marekani, ambapo viongozi hao walijadili masuala ya kusitisha vita kati ya Israel na Hamas pamoja na athari za mashambulizi ya Marekani dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran.
Netanyahu alisema hatua hiyo ya uteuzi ni kwa kutambua mchango wa Trump katika kuendeleza mazungumzo ya amani, hasa kupitia ushirikiano na nchi nyingine kutafuta njia bora ya kuwawezesha Wapalestina kwa mustakabali bora. “Unastahili,” alisema Netanyahu alipomkabidhi Trump barua hiyo. Trump, kwa upande wake, alisema, “Inanigusa sana hasa kutoka kwako.”
Mkutano huo unafanyika katika wakati nyeti ambapo Marekani inatarajiwa kushinikiza Israel kukubali kusitisha mashambulizi Gaza, baada ya vifo vya takribani watu 60,000, wengi wao wakiwa Wapalestina. Maafisa wa Israel na Hamas walikutana Doha, Qatar, kwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, ikiwa ni mara ya kwanza ndani ya wiki sita. Hata hivyo, tofauti bado zipo kuhusu dhamana za usalama na hatma ya Hamas Gaza.
Katika mazungumzo hayo, Netanyahu alisisitiza kuwa Wapalestina “wana haki ya kubaki au kuondoka Gaza kwa hiari yao” akikanusha madai ya Israel kupanga kuwahamisha kwa lazima wakazi wa Rafah. Alisisitiza kuwa Gaza haipaswi kuwa kama gereza, bali sehemu huru inayowapa watu chaguo la maisha bora.
Trump alipohojiwa kuhusu uwezekano wa kuhamishwa kwa nguvu kwa Wapalestina kutoka Gaza, alimwelekeza Netanyahu kujibu. “Inaitwa uhuru wa kuchagua,” alijibu Netanyahu, akiongeza kuwa wanafanya kazi kwa karibu na Marekani kupata mataifa yatakayosaidia ustawi wa Wapalestina.
Trump pia alizungumzia Iran, akisema haamini kuwa kutakuwa na mashambulizi mengine hivi karibuni, akidai Tehran “wanataka kusuluhisha mambo”. Kuhusu Urusi na Ukraine, Trump alisema hana furaha na Rais Putin na aliahidi kurejesha msaada wa silaha kwa Ukraine, akisema: “Tunapaswa kutuma silaha zaidi. Wanapaswa kujilinda.”
Kuhusu suluhu ya mataifa mawili (two-state solution), Trump alielekeza swali hilo kwa Netanyahu, ambaye alisisitiza kuwa Wapalestina wanapaswa kuwa na mamlaka ya kujitawala lakini si ya kuhatarisha usalama wa Israel. “Nadhani tunaweza kufanikisha amani pana na jirani zetu wote tukiongozwa na Rais Trump,” aliongeza Netanyahu.
Uteuzi huu wa Trump kwa Tuzo ya Nobel unakuwa wa pili wa hadhi ya juu, baada ya Pakistan pia kutangaza nia ya kumteua kwa tuzo hiyo mwezi uliopita.
Netanyahu anatarajiwa kuendelea na ziara yake Washington, ambapo atakutana na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, Spika wa Bunge Mike Johnson, na maafisa wengine wakuu wa Marekani.