Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, ametoa wito wa kufanyika kwa mageuzi ya haraka ndani ya Jeshi la Polisi pamoja na kuitishwa kwa mkutano wa kitaifa wa wadau wote ili kujadili ongezeko la mauaji ya waandamanaji nchini humo.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya maandamano ya kitaifa ya Saba Saba yaliyofanyika Jumatatu, Julai 7, 2025, ambayo yaliishia kwa umwagaji damu na vifo vya makumi ya watu, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa vibaya baada ya kukabiliana na polisi.
Ingawa alikuwa akitarajiwa kuongoza maandamano katika Uwanja wa Kamukunji, Odinga hakufika eneo hilo, kwa mujibu wa wasaidizi wake kutokana na vizuizi vya polisi na mapambano yaliyokuwa yakiendelea njiani.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Odinga alieleza kuwa changamoto zinazowakabili Wakenya leo ni zilezile zilizosababisha maandamano ya kihistoria ya Saba Saba mwaka 1990 — ikiwemo hali ngumu ya kiuchumi, gharama kubwa ya maisha, na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu hasa ukatili wa polisi na kukamatwa kiholela kwa raia.
“Tulirithi jeshi la polisi kutoka kwa wakoloni. Linapaswa kufanyiwa mageuzi ili liwe chombo cha kuhudumia wananchi. Huko Tanzania, polisi ni wenye urafiki na hawapendi kutumia risasi ovyo,” alisema Odinga akitoa mfano wa Tanzania kama nchi yenye mfumo wa usalama unaojali utu.
Odinga ameonya kuwa ikiwa ukatili wa polisi dhidi ya raia utaachwa kuendelea, taifa hilo linaweza kujikuta likirudi nyuma katika mafanikio ya kisiasa na kiuchumi yaliyopatikana kwa taabu. Alisisitiza kuwa njia pekee ya kutatua mvutano wa kisiasa na kijamii uliopo kwa sasa ni kupitia majadiliano ya kweli na ya wazi, na si matumizi ya nguvu.
Wito wa Odinga kwa mkutano wa kitaifa unaungwa mkono pia na Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, ambaye hivi karibuni alitoa wito kwa pande zinazohusika kuketi pamoja ili kutafuta suluhu ya kudumu kwa maandamano yanayoendelea. Hata hivyo, Odinga ameweka bayana kuwa nia yake ni kuona mabadiliko ya kimsingi katika mfumo wa usalama, kwa kuhakikisha uwajibikaji wa maafisa wa polisi na kuzuia mauaji ya raia wasio na hatia.
Odinga pia ameonya kuwa iwapo hali hiyo haitadhibitiwa, taifa hilo linaweza kuingia katika kipindi kigumu cha machafuko, kwani “vijana hawawezi kuendelea kuuawa kila mwaka kwa kudai haki zao”, akisisitiza kuwa haki ya kujieleza na kuandamana ni msingi wa demokrasia.