Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Kipchumba Murkomen, ametoa maelekezo mapya kwa maafisa wa polisi kuhusu matumizi ya nguvu na silaha, hasa katika kushughulikia maandamano ya umma, akisisitiza kuwa matumizi ya nguvu yasiwe ya kisasi wala ya kiholela.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika kongamano la Jukwaa la Usalama huko Maralal, Kaunti ya Samburu, Murkomen alizindua sera mpya ya kitaifa inayoweka wazi mwongozo wa kisheria kuhusu jinsi polisi wanavyopaswa kutumia nguvu, akisisitiza kuwa matumizi ya silaha za moto yawe ni suluhu ya mwisho kabisa.
“Nguvu za polisi hazipaswi kutumiwa kama adhabu ya kiholela. Huu sasa ni mwongozo wa kisheria na wa sera, ambao wananchi wanaweza kunishikilia kuwajibika kwa msingi wake,” alisema Murkomen.
Katika mwelekeo huo mpya wa sera, Waziri Murkomen ameelekeza kwamba polisi wataweza kutumia silaha tu endapo kuna sababu za msingi kuamini kwamba mtu anatekeleza au anajiandaa kutekeleza kitendo kinachotishia maisha au kusababisha madhara makubwa, na hakuna njia nyingine ya kuzuia hatari hiyo.
Maagizo hayo yanaeleza kuwa matumizi ya nguvu au silaha yaruhusiwe tu kwa ajili ya kujilinda au kuwalinda wengine dhidi ya tishio la karibu la kifo au majeraha mabaya, pindi mshukiwa anapokamatwa kwa usalama, matumizi ya nguvu zaidi hayaruhusiwi.
Aidha imeagizwa kuwa katika kuvunja mikusanyiko isiyo halali lakini isiyo ya vurugu, polisi hawatakiwi kutumia nguvu. Kama kuna ulazima wa kutumia, iwe kwa kiwango cha chini kabisa.
Waziri huyo amesisitiza kuwa Mkuu wa Polisi nchini Kenya (Inspector General) ameagizwa kuhakikisha kuwa maafisa wote wa Jeshi la Polisi wanapatiwa mafunzo juu ya sheria husika na upeo wa mamlaka yao, na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ndani ya mipaka ya kisheria.
“Hatuwezi kukubali kuona damu ya wananchi inamwagika mitaani kwa sababu ya ukosefu wa mwongozo au nidhamu ndani ya vyombo vya usalama,” alisisitiza.
Murkomen alibainisha kuwa serikali inatekeleza mpango wa kuhakikisha polisi wanapewa vifaa vya kisasa vya kudhibiti misongamano, pamoja na mavazi ya ulinzi kulingana na mazingira hatarishi wanayokabiliana nayo kazini.
Hatua hii inakuja wakati ambapo kunazidi kuwepo malalamiko na mijadala ya kitaifa juu ya matumizi kupita kiasi ya nguvu na visa vya vifo vinavyohusishwa na polisi, hasa katika maandamano ya hivi karibuni kote nchini.