Chama cha ACT Wazalendo kimeilaumu polisi kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kuzuia maandamano na kuvuruga mkutano wao wa kampeni uliofanyika Septemba 6, 2025, mkoani Lindi, huku viongozi wake wakikamatwa na baadaye kuachiwa kwa dhamana.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho iliyotolewa Septemba 7, ACT-Wazalendo ilitoa barua kwa Jeshi la Polisi Septemba 3, kikijulisha azma ya kufanya maandamano kuelekea eneo la mkutano. Hata hivyo, siku ya tukio, polisi waliagiza maandamano yasifanyike na chama kifanye mkutano pekee.
Viongozi wa chama wanasema waliheshimu agizo hilo ili kuepusha kusitishwa kwa mkutano, lakini baada ya mkutano kumalizika, wanachama waliokuwa wakitoka maeneo ya mbali walipoandamana kuelekea ofisi za chama kwa ajili ya maandalizi ya usafiri, polisi walitafsiri kitendo hicho kama maandamano haramu na kutumia mabomu ya machozi bila kutoa tahadhari, hali iliyosababisha taharuki na majeruhi.
Katika tukio hilo, viongozi kadhaa walikamatwa, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara na mgombea ubunge Jimbo la Lindi Mjini, Isihaka Mchinjita ambaye amelitaka Jeshi la Polisi kufanye kazi kwa weledi na kutoa nafasi kwa wananchi kuwasikiliza wagombea.
“Tunamtaka IGP Wambura kuhakikisha polisi wa Lindi wanakuwa na uwezo na uadilifu. Polisi wajitenge na siasa. CCM wametuhujumu vya kutosha, wasitengeneze mazingira ya kutufanya tuwakabili kama tunavyokabiliana na CCM,” amesema Mchinjita.
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi, kupitia taarifa yake ya Septemba 7, lilikiri kumkamata Mchinjita na wafuasi sita, likibainisha kuwa ACT Wazalendo iliomba kufanya maandamano ya kilomita nne kuelekea viwanja vya Mpilipili kwa mkutano wa kampeni, lakini ombi hilo lilikataliwa.
Polisi walisema kuwa baada ya mkutano kumalizika majira ya saa 12 jioni, viongozi na wanachama wa chama hicho walianza maandamano licha ya katazo, hivyo polisi wakalazimika kutumia nguvu kuyavunja na kuwakamata wahusika.
“Jeshi la Polisi lililazimika kutumia nguvu ya kadri kuwatawanya waandamanaji hao sambamba na kufanikiwa kumkamata Makamu Mwenyekiti Taifa Ndugu Isihaka Mchinjita na wenzake Sita. Baada ya kukamatwa walihojiwa na kuachiwa kwa dhamana wakisubiri hatua nyingine za kisheria zitakazofuata. ilieleza taarifa ya polisi”, imeeleza taarifa ya polisi.
Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi alitoa wito kwa vyama vya siasa na wananchi kuzingatia sheria na taratibu za uchaguzi, akisisitiza kuwa polisi hawatasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayeshiriki au kushawishi uvunjifu wa amani.