Latest Posts

POLISI WATHIBITISHA VIFO 11 NA MAMIA KUKAMATWA KUFUATIA MAANDAMANO YA SABA SABA NCHINI KENYA

Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) nchini Kenya imethibitisha vifo vya watu 11 na majeruhi 63 wengine kutokana na maandamano ya kitaifa ya Saba Saba yaliyofanyika Jumatatu, Julai 7, 2025.

Katika taarifa iliyotolewa jioni ya siku hiyo, msemaji wa polisi Muchiri Nyaga alisema kuwa kati ya waliojeruhiwa, maafisa wa polisi ni 52 huku raia wakiwa 11, na jumla ya watu 567 walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa magari 19 yaliharibiwa wakati wa maandamano hayo – yakiwemo magari 12 ya polisi, magari 3 ya serikali na magari 4 ya kiraia. Maandamano hayo yameacha athari kubwa za uharibifu, taharuki na hali ya wasiwasi miongoni mwa wananchi na wafanyabiashara katika miji mbalimbali.

“Tunawashukuru Wakenya waliotii wito wa kutunza amani, lakini pia tunalaani makundi madogo ambayo yalidhamiria kuvunja sheria kwa kushambulia maafisa wa usalama na kujihusisha na uporaji,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya NPS. Huduma hiyo ilisisitiza kuwa matukio yote yaliyorekodiwa yatachunguzwa kwa kina na wahusika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Wakati polisi wakijipongeza kwa kile walichokiita “kiasi kikubwa cha uvumilivu na weledi” wakati wa maandamano, mashirika ya haki za binadamu yameanza kutoa takwimu na ripoti zinazoashiria kiwango kikubwa cha ukatili wa vyombo vya dola.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) hadi kufikia saa 12 jioni ilikuwa tayari imethibitisha vifo 10, majeruhi 29, utekaji wawili wa raia na kukamatwa kwa watu 37 katika kaunti 17 tofauti. Miongoni mwa waathirika waliripotiwa kupigwa risasi, kushambuliwa kwa virungu na wengine kupotea kwa muda kabla ya kurejea kwao wakiwa na majeraha ya kuogofya.

Kwa upande wake, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen aliahidi kuwa wote waliohusika na vurugu, uchochezi au uharibifu watachunguzwa na kufikishwa mahakamani. “Serikali haitaruhusu watu wachache kuvuruga amani ya nchi,” alisema Murkomen huku akiwapongeza polisi kwa “uamuzi mzito na wa kiusalama waliouchukua kulinda maisha ya raia.”

Maandamano ya Saba Saba mwaka huu yamekuja kuadhimisha miaka 35 tangu kuanzishwa kwa harakati za kudai demokrasia nchini Kenya mnamo Julai 7, 1990. Hata hivyo, mwaka huu yameibua kumbukumbu chungu kutokana na kiwango cha maafa, mateso na hofu miongoni mwa wananchi hasa vijana.

Mitaa mingi ya Nairobi, Mombasa, Kisumu na Eldoret ilishuhudia misururu ya vizuizi vya polisi na magari ya usalama yakizuia upitaji, huku biashara nyingi zikifungwa kwa hofu ya uporaji. Ripoti kutoka kaunti kama vile Kakamega, Nyeri, Homa Bay, Laikipia na Machakos zilithibitisha matukio ya uporaji wa maduka na majeruhi wa risasi.

Mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu na mabalozi wa mataifa ya Magharibi tayari wameeleza wasiwasi wao kuhusu kiwango cha nguvu kinachotumiwa na polisi, wakitaka uchunguzi wa kina na haki kutendeka kwa waathirika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!