Wananchi Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro wameeleza kumuonesha jeuri Mgombea wa Ubunge Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe kwa kumridhia kuongoza jimbo hilo katika uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Wananchi hao wameeleza kuwa jeuri hiyo ni ya kuwakatalia wagombea wengine kuwaongoza kutokana na changamoto zilizokuwa zinakabili jimbo hilo kutatuliwa na Saashisha Mafuwe katika kipindi cha miaka mitano alichowaongoza.
Akizungumza Septemba 5,2025 katika Mkutano wa kutambulishwa Madiwani 17 watakao gombea uliofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Harambee Kata ya Machame Kaskazini, na Kata ya Kia
Mgombea ubunge wa Jimbo la Hai kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Saashisha Mafuwe, ameahidi kutumia ushawishi na mahusiano yake ndani ya Serikali kuhakikisha soko la mnada la mifugo ililopo eneo la Mijohoroni, Kata ya Kia, linajengwa kwa kiwango cha kisasa ili kuwawezesha wafugaji kuuza mifugo yao katika mazingira bora na yenye tija.
Saashisha
Amesema ujenzi wa soko hilo ni moja ya kipaumbele chake ikiwa atapata ridhaa ya wananchi kurejea bungeni, kwa kuwa linahusiana moja kwa moja na kuinua kipato cha jamii ya wafugaji wilayani humo.
“Najua hapa mlipo soko hili bado halijafanana na Wilaya hii lazima tutengeneze mazingira ya soko hili likae kwa mfumo wa kuwa soko linalofanana na Wilaya ya Hai,”amesema Mafuwe
Ameongeza kuwa ikiwa Wananchi wa Jimbo hilo watampigia kura za kishindo atahakikisha anainua uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa kwa Wananchi.
“Ikiwa CCM itapata ridhaa kwa kumchagua Dkt.Samia Hassan kuwa Rais na mimi kuwa Mbunge pamoja na kuwachagua Madiwani wa CCM nitahakikisha uchumi wa mtu mmoja mmoja unakuwa kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri katika kilimo cha uhakika,maji na miundombinu ya barabara kuchochea uchumi huo”
Aidha, Mafuwe amewaomba wananchi hao kuendelea kumuamini na kumpa ridhaa ya kuendelea kuliongoza Jimbo hilo kwa kipindi cha pili huku akitolea mfano miradi ambayo ameitekeleza ikiwemo ya miradi ya maji.
“Wakati naingia hapa Wilaya ya Hai, kulikuwa na tatizo kubwa la maji, nikapambana nikapata Sh3.39 bilioni leo wenzetu wa Bomang’ombe wana maji, na wananchi wetu wa Kia kihistoria tulikuwa hatuna maji na leo tuna maji,”amesema Mafuwe
Amesema”Pesa za matengenezo ya barabara wakati naingia ilikuwa Sh1 bilioni leo ni sh6.9 bilioni maana yake tumeweza kupata fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara zetu, ninyi ni mashahidi barabara zetu za Kia zimejejengwa na zinapitika.”
Akizungumza katika mkutano huo, Felista Njau, ambaye alikuwa mtiania wa ubunge Jimbo Moshi vijijini, amesema wananchi wa jimbo la Hai wanacho cha kujivunia kwa kuwa walimpata kiongozi muwajibikaji na kuwataka wasifanye makosa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
“Wananchi wa Hai mna kijana mpambanaji, mshikilieni hakikisheni Oktoba 29 mnampigia kura za kutosha ili aendelee kuwapambania kuwaletea maendeleo zaidi,”amesema Njau
Akizungumzia changamoto ya soko hilo, Baraka Lazier amesema soko hilo halina miundombinu ya kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira rafiki.