Latest Posts

SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZAMIMINIKA KWA KIFO CHA RAIS WA ZAMANI WA NIGERIA

Salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi wa mataifa mbalimbali, taasisi za kikanda na kimataifa zinaendelea kumiminika kufuatia kifo cha Rais wa zamani wa Nigeria, Muhammadu Buhari, aliyefariki dunia Jumapili katika kliniki moja jijini London akiwa na umri wa miaka 82.

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imetoa pole kwa serikali na wananchi wa Nigeria, ikimtaja marehemu Buhari kuwa ni “mwanasiasa mashuhuri ambaye mchango wake uliendeleza demokrasia na mshikamano wa kikanda barani Afrika.”

Katika salamu zake, Rais wa Tume ya ECOWAS, Omar Alieu Touray, amesema: “Buhari alikuwa kiongozi aliyekuwa imara katika misingi ya utawala wa sheria na mshikamano wa Afrika Magharibi.”

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ameungana na waombolezaji kwa kusema: “Tunasimama na Nigeria katika kipindi hiki kigumu. Rais Buhari alikuwa mzalendo na bingwa wa matumaini ya baadaye ya taifa lake.”

Makamu wa Rais wa zamani wa Nigeria, Atiku Abuja, ameelezea marehemu kama mtu aliyejitolea maisha yake yote kwa ajili ya ustawi wa Nigeria: “Alijitambulisha kwa nidhamu na uzalendo wa kweli.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), aliyekuwa ameomba apone haraka saa chache kabla ya taarifa za kifo chake, alisema kupitia mitandao ya kijamii: “Nimepokea habari hizi kwa huzuni kubwa. Buhari alikuwa kiongozi aliyepigania mustakabali wa Afrika kwa moyo wa dhati.”

Viongozi wengine waliotoa salamu za pole ni pamoja na Rais wa Sierra Leone, Julius Maada Bio, ambaye alitaja kifo cha Buhari kama “hasara mbaya”, pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, aliyesema marehemu atakumbukwa kwa “uadilifu, kanuni thabiti na heshima kubwa kwa taifa lake.”

Rais wa zamani wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Akinwumi Adesina, naye ameungana na waombolezaji kwa kusema: “Namshukuru kwa uzalendo na huduma yake ya dhati kwa taifa la Nigeria.”

Viongozi wa zamani wa Nigeria pia wameelezea huzuni zao, akiwemo Goodluck Jonathan aliyemtaja Buhari kama “kiongozi aliyeitumikia nchi kwa moyo wa kujitolea bila ubinafsi”, na Olusegun Obasanjo aliyesema kifo hicho ni pigo kwa taifa.

Mtawala wa zamani wa kijeshi wa Nigeria, Jenerali Ibrahim Babangida, pia amemwagia sifa Buhari kwa mchango wake kwa taifa na jeshi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!