Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Kenya, Kipchumba Murkomen, amewapongeza maafisa wa polisi kwa kazi yao ya kudumisha utulivu na kupunguza ghasia wakati wa maandamano ya kuadhimisha Siku ya Saba Saba, yaliyofanyika jijini Nairobi siku ya Jumatatu.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa baada ya kutembelea maeneo kadhaa ya jiji hilo, Murkomen alisema kuwa maafisa hao walionesha kiwango cha juu cha kujitoa katika kulinda maisha na mali ya wananchi, licha ya changamoto zilizojitokeza wakati wa maandamano hayo.
“Utendaji wao ni wa kupongezwa na muhimu kwa usalama wa umma,” alisema Murkomen.
Siku ya Saba Saba huadhimisha miaka 35 ya harakati za demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya, lakini maandamano ya amani ya mwaka huu yaliripotiwa kuvurugwa na baadhi ya watu waliotuhumiwa kuanzisha vurugu na uharibifu wa mali, huku watu 11 wakiripotiwa kuuawa.
Waziri huyo alieleza kuwa kulikuwa na upungufu mkubwa wa fujo ikilinganishwa na maandamano ya Juni 25, ambapo ghasia zilienea kwa kasi na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za umma na binafsi.
“Maandamano ya Saba Saba ni ya kihistoria, yanapaswa kuadhimishwa kwa amani na nidhamu. Hata hivyo, baadhi ya wahalifu wamekuwa wakitumia fursa hiyo kusababisha vurugu,” alisema Murkomen.
Ameongeza kuwa wote waliohusika katika uvunjifu wa amani watachunguzwa na kufunguliwa mashtaka, kama ilivyofanywa kwa waliokamatwa katika maandamano ya awali.