Serikali kupitia Wizara ya Madini imetangaza rasmi orodha ya Huduma na Bidhaa 20 zinazopaswa kutolewa Migodini kupitia kampuni zinazomilikiwa na watanzania kwa asilimia 100 ikilenga kuongeza wigo wa ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kuhakikisha watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzimawa sekta ya madini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde Januari 5, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari na kueleza kuwa, hatua hiyo  imefanyika baada ya kufanywa marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta ya Madini za Mwaka 2018.
‘’Kwa awamu ya kwanza tarehe 14 Novemba, 2025 Tume ya Madini ilitangaza orodha ya bidhaa na huduma zinazotakiwa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa na kampuni za kitanzania kwa asilimia 100, ambapo kwa mara ya kwanza Tume ya Madini itatatangaza kupitia Kanuni 13A,’’ amesema Waziri Mavunde.

Akizungumzia manunuzi ya huduma na bidhaa kwa kampuni za kitanzania amesema yameongezeka kutoka kiasi cha Shilingi trilioni 1.85 kati ya manunuzi ya huduma na bidhaa za jumla ya kiasi cha Shilingi trilioni 3.01 sawa na asilimia 62 kwa mwaka 2018 hadi kufikia Shilingi trilioni 4.41 ambayo ni sawa na asilimia 88 ya kiasi cha Shilingi trilioni 5.00 ya manunuzi yote yaliyofanyika mwaka 2024.
Kwa upande wa ajira kwenye miradi ya madini, amesema kumeshuhudiwa ongezeko la ajira kwa watanzania kutoka ajira 6,668 kati ya ajira 7,003 sawa na asilimia 95 kwa mwaka 2018 hadi kufikia ajira 18,853 kati ya ajira 19,356 sawa na asilimia 97 kufikia Desemba 2024.
‘’katika nafasi zinazohitaji kupata uzoefu kutokana na kukua kwa teknolojia duniani, kumekuwa na utaratibu wa kisheria wa urithishwaji wa Watanzania kwa nafasi zinazoshikiliwa na Wataalamu wa Kigeni,’’ na kutolea  mfano wa mgodi wa dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya Twiga Minerals Corporation (Barrick Gold) ambapo nafasi zote za juu za uongozi zinashikiliwa na Watanzania kwa asilimia 100.
Samamba na hayo, amesema Serikali inaendelea kufungua wigo kwa ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini na kuongeza manufaa ya rasilimali madini kwa kutenga eneo maalum la uwekezaji la ulipokuwa Mgodi wa uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu la Buzwagi lenye ukubwa wa ekari 1331, kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za migodini na kusema tayari viwanda sita vimekwisha jengwa huku wamiliki wa viwanda 15 wakionesha nia ya kujenga viwanda katika eneo hilo.
Waziri Mavunde ameitaka sekta binafsi nchini Tanzania kuchangamkia fursa ya usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma migodini ili kuhakikisha fedha kiasi kikubwa inabaki nchini Tanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Amewasisitiza wawekezaji wote kuzingatia Sheria za madini na utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji Watanzania kwenye sekta ya madini sambambamba na kuwataka watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika miradi ya madini ili kukabiliana na changamoto za ajira kwa manufaa ya mtu mmoja mmoja na manufaa ya taifa.