Sheikh Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amewataka Waislamu na Watanzania kwa ujumla kuutumia Mwezi Mtukufu wa Ramadan kama fursa ya kuimarisha umoja, mshikamano na amani ndani ya jamii.
Akizungumza na Jambo Tv, Sheikh Kabeke amesema mkoa huo umeendelea kuwa tulivu bila kuwepo kwa migogoro na kelele zisizo za lazima ndani ya misikiti, madrasa na taasisi mbalimbali za Kiislamu akisisitiza kuwa utulivu huo unapaswa kuendelezwa zaidi katika mwezi wa Ramadan.
“Mwezi wa Ramadan ni mwezi wa kusameheana, kuomba msamaha kwa Mola, ni mwezi wa subira, kutoa sadaka, kusaidia wasiojiweza, wajane, yatima, ni mwezi wa hisani na fadhila nyingi na ni mwezi wa kukithirisha kufanya ibada, kusoma Quran, kumswalia mtume nakadharika,” amesema

Katika hatua nyingine, Sheikh Kabeke amesema uongozi wa BAKWATA Taifa umeupendekeza Mkoa wa Mwanza kuwa eneo la uzinduzi wa mfumo wa kitaifa wa database ya madrasa zote nchini, zitakazojumuisha madrasa zilizo chini ya BAKWATA na zile zisizo chini ya baraza hilo.
Amesema uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Februari 24, 2026 na utaongozwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dk Abubakar Zubeir Bin Aly ambaye pia atazindua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za BAKWATA Mkoa wa Mwanza.
“Ni jambo la kihistoria kwa mkoa wetu kupokea uzinduzi huu muhimu pamoja na ujio wa Mufti, hatua itakayosaidia kuimarisha usimamizi na maendeleo ya madrasa pamoja na shughuli za BAKWATA kwa ujumla,” amesema Sheikh Kabeke.