Katika hali isiyo ya kawaida, sintofahamu iliibuka Septemba 10, 2025 wakati wa siku ya kwanza ya kampeni za Mgombea Urais wa Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Tabora zilizofanyika Wilayani Nzega, baada ya mabango yaliyokuwa yakimnadi mgombea huyo kuondolewa ghafla kabla ya ujio wake.
Mabango hayo yametaja kuandaliwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Nzega Vijijini, Dkt. Hamisi Kigwangalla, yakionesha miradi na kazi zilizotekelezwa na CCM chini ya uongozi wa Dkt. Samia katika jimbo hilo na wilaya nzima. Hata hivyo, inadaiwa kuwa viongozi wa chama katika Wilaya ya Nzega walimpigia simu Kigwangalla na kumtaka kuyaondoa kwa madai kuwa yeye si mgombea, hivyo hapaswi kutengeneza mabango ya kumnadi mgombea wa Urais.
Kwa mujibu wa mashuhuda na waandishi waliokuwepo Tabora, mabango hayo yalikuwa yanaonekana dhahiri mapema asubuhi ya tarehe 10 Septemba, lakini yaliondolewa kufikia mchana.
Taarifa ambazo Jambo TV imezipata zinaeleza kuwa Kigwangalla alitetea hatua yake akisema yeye kama mwana CCM ana haki na wajibu wa kumuombea kura mgombea wa urais kupitia chama chake. Hata hivyo, viongozi wa chama wilayani humo walimtaka abadilishe mabango hayo na kuweka pia picha za mgombea ubunge aliyeidhinishwa kwa jimbo hilo, jambo alilokataa. Baada ya mvutano huo, maofisa usalama wa Wilaya wakaamuru mabango hayo yaondolewe mara moja.
Mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio walimuona mmoja wa viongozi wa usalama wilaya ya Nzega, ambaye alijulikana kwa jina moja tu la Michael akichanachana kwa kisu bango moja lililokuwepo eneo la Tabora Road, Nzega Mjini. Hata hivyo, Jambo TV ilipomtafuta kwa njia simu alikata simu hiyo mara tu alipogusiwa suala hilo na alipotafutwa tena alipokea na kukata tena simu hiyo.
Jambo TV imemtafuta pia kwa njia ya simu Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega, Adia Rashid ambaye ameeleza kuwa hatua ya kuondolewa kwa mabango hayo ilihusiana moja kwa moja na kutokufuata utaratibu wa chama.
“Hilo bango ambalo mimi nimeliona pia ni la picha ya mgombea wetu wa Urais lakini ikawekwa ‘logo’ ya Kigwangalla ya HK, maana yake nini? Utaratibu wa mwanachama wa kawaida kumnadi mgombea ni lazima upitie kwenye chama, kamati ya siasa ndiyo kamati ya kampeni kwahiyo kikao cha kamati ndicho kinachoelekeza kwamba chama mnatakiwa kufanya hivi, na mwanachama pia kama anataka kutoa msaada anapitia kwenye chama, chama ndicho kinatoa maelekezo. Kwahiyo kama mwanachama ana kitu chochote kile kwa mfano anataka kuleta sare, anataka kusaidia mafuta, anataka kuleta mabango, analeta kwenye chama, chama ndicho kinatekeleza …yaaani unaleta ofisi ya CCM, tunaitaarifu kamati ya siasa, mdau wetu fulani au mbunge wetu wa zamani kaleta kitu fulani tunafanyia kitu fulani. Kwahiyo ni utaratibu tu haujafuata kama yeye ameamua tu kuweka bango, lazima kila kitu kifuate utaratibu”, ameeleza.
Adia ameongeza kuwa kila bango linalowekwa kipindi cha kampeni lazima liwe na idhini ya chama.
“Kwahiyo mabango yote ya chama unayoyaona yamewekwa kwa utaratibu, na yote yanasimamiwa na Chama Cha Mapinduzi kama ni ngazi ya wilaya mimi ndiye Mtendaji Mkuu. Kwa mfano wagombea wangu wote hapa mjini wametengeneza mabango: Mjini, Bukene, Vijijini, picha nimewaelekeza kwamba picha inayohitajika ya mgombea wetu wa Urais ni hii na picha zao zinazohitajika wamenitumia nikazikagua nikawaambia sawa hizi ndizo zitumike, kwahiyo kila kitu kilifuata utaratibu”.
Naye Dkt. Kigwangalla alipopigiwa simu amesema mabango hayo aliyatengeneza kwa ridhaa ya chama Makao Makuu, na kwamba picha alizoweka ni zile alizopewa na chama. Aidha, mratibu wa kampeni za CCM Kanda ya Kati, Dkt. Bashiru Ally Kakurwa aliridhia yawekwe na alielekeza kwamba ‘logo’ ya HK ifunikwe na stika- maelekezo aliyoyatii. Pamoja na kutii maelekezo hayo ameshangazwa kuona mabango yake yote yakitolewa.
Hata hivyo Dkt. Kigwangalla anakiri kuombwa na chama wilaya ya Nzega kutumia miundombinu yake ya kampeni na kwamba anadai walichelewa kumuomba kwa kuwa alikuwa amekwishaandaa mabango yake mwenyewe na aliwaahidi kuwapa wayatumie baada ya Mgombea Urais kupita.
Tukio hilo la Kigwangalla linahusishwa na mvutano wa muda mrefu ndani ya CCM kutokana na kura za maoni za ubunge zilizofanyika mwezi uliopita. Katika mchakato huo, Kada wa CCM, Neto Kapalata, aliibuka mshindi kwa kura 2,570, akimshinda Kigwangalla aliyepata kura 1,715, huku CPA Robert Masegere akipata kura 1,635. Kushindwa kwa Kigwangalla kulihusishwa na njama za kisiasa zinazodaiwa kufanywa na baadhi ya vigogo wa chama hicho wilayani Nzega