Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limezindua rasmi matumizi ya ndege nyuki (drone) yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 70 kwa ajili ya kufukuza tembo wanaovamia makazi ya wananchi na mashamba, ikiwa ni jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha usalama wa wananchi na mazao yao.
Akizungumza katika Kijiji cha Kisaki mkoani Morogoro, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ephraim Mwangomo, alisema droni hiyo ina uwezo wa kuruka umbali wa zaidi ya kilometa 15 na itamaliza adha ya wananchi kuvamiwa na tembo. Alisisitiza kuwa teknolojia hiyo ni salama na haina madhara kwa askari wa doria wala wananchi.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki Fredrick Malisa, alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli za kilimo kwa uhakika na bila hofu ya wanyama waharibifu.
Naye Mtendaji wa Kata ya Kisaki, Raymond Mwakilema, alisema vijiji vilivyokuwa vikikumbwa na changamoto ya tembo ikiwemo Kichangani, Gomero na Nyarutanga sasa vimepata suluhisho la kudumu kutokana na teknolojia hii mpya.
Wananchi akiwemo Athumani Ally, Rehema Yusufu na Kuruthum Nyeya waliipongeza Serikali kwa hatua hiyo, wakisema imekuwa chachu ya kuimarisha uchumi wa kaya na Taifa kwa ujumla. Walisema sasa wana uhakika wa kulima na kuvuna bila hofu ya tembo kuvamia mashamba yao.
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) linaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia bunifu katika kusimamia hifadhi na kuhakikisha wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi wanaishi kwa amani na usalama.