Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotarajiwa kufaidika na fedha hadi dola milioni 20 (takriban Shilingi bilioni 49) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya mikataba ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.
Akizungumza hivi karibuni katika mkutano maalumu na Watanzania wanaoshiriki Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30) unaoendelea mjini Belem, Brazil, Mshauri wa Rais katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN), Dkt. Richard Muyungi, amesema mfuko huo tayari umepangwa kuanza kutekelezwa mwaka 2026.

Dkt. Muyungi alisema kuwa katika utekelezaji huo, fedha kiasi cha dola milioni 250 tayari zimetengwa kwa ajili ya kusaidia nchi zinazoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, ambapo Tanzania imepewa nafasi ya kuwasilisha miradi itakayonufaika na ufadhili huo.
Amesisitiza kuwa fedha hizo si mkopo bali ni ruzuku kamili yenye lengo la kusaidia mataifa yanayoathiriwa zaidi na tabianchi kujiimarisha kimazingira, kiuchumi na kijamii.
“Tumepewa nafasi ya pekee kama moja ya nchi zinazopewa kipaumbele. Tunaweza kuwasilisha miradi miwili mikubwa na tukapata ufadhili wote. Hii si fedha ya kurudisha, ni ruzuku,” alisema Dkt. Muyungi.

Amefafanua kuwa ili kufanikisha ushiriki wa Tanzania katika mfuko huo, ni muhimu kwa serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuteua mtu maalumu atakayekuwa kiunganishi wa kushughulikia taratibu zote za mfuko huu kwa niaba ya nchi.
Akiwasilisha wito kwa Watanzania wanaoshiriki mkutano huo, Dkt. Muyungi amewataka kutumia fursa ya uwepo wa washiriki zaidi ya 60,000, wakiwemo wawakilishi wa taasisi za kifedha, serikali na mashirika ya kimataifa, katika kujenga mitandao na kusaka fursa za maendeleo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Prof. Peter Msoffe, amesema ujumbe wa Tanzania umefika Belem kama timu yenye malengo ya pamoja, kuhakikisha haitoki mikono mitupu.

“Nawaomba tuendelee kushirikiana. Kila mmoja akiona fursa ambayo haiwezi kufanyiwa kazi na yeye, amwambie mwenzake. Tunafanya kazi kama timu. Lengo ni kuhakikisha tunarudi na manufaa kwa Taifa,” amesema Prof. Msoffe.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban, amesema lengo kuu la ujumbe wa Tanzania ni kusaka rasilimali za kugharamia mipango ya mazingira, ikiwemo fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni.

“Mipango yote tunayoweka ina thamani pale tu inapoleta fedha. Ndiyo maana tuko hapa, kusaka fedha hizo kupitia fursa zilizopo. Tukiwa na miradi iliyoandaliwa vizuri, sisi tupo tayari kuitafutia fedha,” amesema.
Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu ni mfuko unaolenga kusaidia nchi zinazoathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi, hususan mataifa ya Afrika, Asia na visiwa vidogo. Tofauti na mifuko mingine, mfuko huu unahusika na hasara za kiuchumi kama uharibifu wa mali, kilimo na miundombinu, pamoja na hasara zisizo za kiuchumi ikiwemo vifo, uhamaji, athari za kisaikolojia, tamaduni na kumbukumbu za kijamii.
Afrika, ikiwa imeathirika na majanga zaidi ya 1,600 yanayohusishwa na tabianchi, imekuwa ikiangaliwa kama bara linalohitaji msaada wa dharura, licha ya kuchangia kwa kiwango kidogo sana katika uzalishaji wa hewa ukaa au gesi joto duniani kwani mataifa makubwa, mengi yakiwa ukanda wa juu wa dunia ndiyo huchangia kwa kiasi kikubwa gesi hizo hivyo kuathiri moja kwa moja mataifa ya ukanda wa chini.
Tanzania inaingia kwenye mfuko huu katika wakati ambapo inaendelea kutekeleza mipango ya kitaifa ya kukabiliana na tabianchi, ikiwemo programu za kilimo himilivu, uhifadhi wa vyanzo vya maji, kukabiliana na ukame, mafuriko na mmomonyoko wa ardhi.