






Zanzibar
Katika kuendeleza ushirikiano na wadau wa Sekta ya Elimu nchini, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF Tanzania) wamefungua rasmi milango ya utekelezaji wa miradi ya elimu visiwani Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA), kwa lengo la kuboresha miundombinu ya elimu.
Kupitia ushirikiano huo, TEA na UNICEF wametenga jumla ya shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa vyumba vya madarasa, maabara za sayansi pamoja na matundu ya vyoo katika shule 20 ambapo, shule 11 zipo kisiwani Unguja na shule 9 kisiwani Pemba.
Akizungumza wakati wa kikao kazi maalum cha kujadili utekelezaji wa miradi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha alisema, utekelezaji wa mradi unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Januari na kukamilika kabla ya mwezi wa sita mwaka huu.
Dkt. Kipesha alibainisha kuwa lengo la mradi huo ni kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora, salama na rafiki kwa afya zao. Aliongeza kuwa TEA ni taasisi ya Muungano hivyo utekelezaji wa miradi ya elimu Zanzibar ni sehemu ya majukumu yake ya msingi.
Aidha, alisisitiza kuwa ushirikiano uliopo kati ya TEA na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar umekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya miradi mbalimbali ya elimu inayotekelezwa na ambayo imekamilika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw. Khamis Said, aliishukuru TEA kwa mchango mkubwa kwenye uboreshaji wa miundombinu ya elimu huku akieleza kuwa miradi hiyo imekuwa kichocheo cha wadau wengine kujitokeza kusaidia maendeleo kwenye sekta ya elimu.
Bw. Said aliongeza kuwa ukarabati na ujenzi wa miundombinu hiyo umefika wakati muafaka kwani majengo mengi ya shule hizo ni ya kizamani na yako katika hali isiyoridhisha. Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutachangia kuinua kiwango cha taaluma kwani wanafunzi watapata motisha ya kusoma katika mazingira ya kisasa.
“Wizara inatoa shukrani za dhati kwa TEA kwa ushirikiano mkubwa mnaoendelea kutupatia katika kuboresha miundombinu ya elimu na tunawaahidi kusimamia utekelezaji wa miradi yote kwa ufanisi ili ilete tija kwa maendeleo ya sekta ya elimu,” alisema Bw. Said.
Kwa sasa TEA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu ya elimu Zanzibar kama taasisi ya Muungano. Awali, jumla ya shilingi bilioni 3.2 zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mafunzo ya amali ambayo utekelezaji wake bado unaendelea huku shilingi bilioni 2.5 zikitengwa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa madarasa, maabara za sayansi na matundu ya vyoo.