Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wamekutana Mjini Morogoro kwa kikao cha siku mbili kuanzia Septemba 11 hadi 12, 2025. Kikao hiki kinafanyika kwa lengo la kupitia na kujadili masuala ya kiutumishi pamoja na hali ya utekelezaji wa miradi ya elimu kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025.
Kikao hicho cha Tano kwa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa TEA kinaongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la TEA ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka Dkt. Erasmus Kipesha.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kipesha amesisitiza kuwa kikao hicho kinatarajiwa kutoa mchango muhimu katika kupanga mikakati ya kuboresha mazingira ya kazi na utekelezaji wa majukumu ya TEA.
Kupitia kikao hicho, wajumbe watapata fursa ya kutoa maoni, mapendekezo na tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Mamlaka, sanjali na kuimarisha ushirikiano kati ya menejimenti na watumishi. Aidha, kikao hicho ni sehemu ya utaratibu wa kisheria unaolenga kukuza uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi ya kiutendaji na utekelezaji majukumu mbalimbali ya Mamlaka.