





Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) leo imeshiriki katika maonyesho maalum yaliyoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA) kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Wataalamu wa Uhasibu. Maonyesho hayo yamefanyika katika viwanja vya jengo la Mhasibu Posta, jijini Dar es Salaam.
Ushiriki wa TEA katika maonyesho hayo ni sehemu ya jitihada za Mamlaka katika kutangaza shughuli zake pamoja na kuimarisha uhusiano na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu kutoka taasisi tofauti.
Kupitia maonyesho hayo, TEA ilitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu ya Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na Mamlaka hiyo pamoja na mchango wa mfuko huo katika kusaidia jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia nchini.
Akizungumza wakati wa maonyesho hayo Afisa Mawasiliano wa TEA Bi. Eliafile Solla, aliwahimiza wadau wa elimu kushirikiana na Mfuko wa Elimu wa Taifa kwa kutoa michango mbalimbali itakayoongeza uwezo wa mfuko huo kufadhili miradi ya elimu katika maeneo mbalimbali nchini.
Bi. Solla alisema kuwa, lengo kuu la Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na TEA ni kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora na kwa usawa bila kujali mazingira au hali ya kiuchumi anayotoka.
Kutokana na ushiriki wake mahususi na mchango wake katika maonyesho hayo, Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA) imeitunuku Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) cheti maalum cha shukrani na utambuzi.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni taasisi ya umma iliyo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inayosimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa wenye lengo la kukusanya rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara za Sayansi na nyumba za walimu, ili kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa usawa nchini.