Latest Posts

TPDC YAHAMASISHA JAMII KULINDA MIUNDOMBINU YA GESI KWA BONANZA LA MICHEZO NANGURUWE

Katika kuhamasisha wananchi kuendelea kulinda miundombinu ya gesi asilia inayopatikana katika eneo la Ntorya, Kata ya Nanguruwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limefanya bonanza la michezo kwa kushirikisha timu mbalimbali kutoka katika kata halmashauri hiyo.

Bonanza hilo lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nanguruwe limekutanisha timu nane, ambapo timu zilizoshika nafasi tatu za juu ni Watumishi FC, Ngome FC na Mafundi FC.

Akizungumza wakati wa bonanza hilo, Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya, amesema kuwa lengo kubwa la TPDC ni kuendelea kuwa karibu na jamii, ikizingatiwa kuwa kuna uwekezaji mkubwa unaoendelea katika halmashauri hiyo.

Ameeleza kuwa uwekezaji huo utawanufaisha wananchi wote na kutoa rai kwao kuendelea kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa miradi inayotarajiwa kufanyika katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka TPDC Ally Mluge, amesema kuwa Nanguruwe ni moja ya maeneo ambayo gesi asilia itaanza kuzalishwa, baada ya kugunduliwa kiasi cha futi za ujazo trilioni 1.6, hivyo kufanya eneo hilo kuwa sambamba na maeneo ya Msimbati na Songosongo katika uzalishaji wa gesi nchini.

Ameongeza kuwa TPDC inatarajia kuanza ujenzi wa bomba la gesi kutoka visima vya Ntorya hadi Madimba, kwenye kiwanda cha kuchakata gesi, na kwamba bonanza hilo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya TPDC na jamii.

Timu zilizoshiriki bonanza hilo ni ,Mafundi FC, Chitenda Hamu, Bodaboda FC, Mtemba City, Ajaksi Ngolongolo, Tandika FC, Ngome FC na Watumishi FC, ambapo Watumishi FC waliibuka mabingwa baada ya kuifunga Ngome FC, huku Mafundi FC wakitwaa nafasi ya tatu.

Washindi wa bonanza walizawadiwa kombe, jezi, mipira na glovu kulingana na nafasi zao, huku timu zote zikipewa zawadi. Wananchi wamepongeza bonanza hilo kwa kuongeza umoja na kuwainua wajasiriamali wadogo pamoja na kujiandaa na fursa zinazotarajiwa kujitokeza kutokana na miradi ya gesi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!