Rais wa Marekani, Donald Trump, ametoa onyo kali kwa mataifa yote duniani yanayofanya biashara na Iran, akitangaza kuwa nchi yoyote inayoendelea na itakayofanya hivyo itakabiliwa na ushuru mpya wa asilimia 25 kwa bidhaa zake zote zinazouzwa nchini Marekani.
Hatua hiyo imekuja wakati utawala wa Trump ukishinikiza Iran kusitisha kile ilichokiita ukandamizaji dhidi ya waandamanaji wanaopinga serikali ya kidini nchini humo. Kupitia chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii, Trump amesisitiza kuwa agizo hilo ni la mwisho na la lazima, akiongeza shinikizo la kiuchumi sambamba na vitisho vyake vya awali vya kuchukua hatua za kijeshi.
“Agizo hili ni la mwisho na la hitimisho,” amesema Trump, hatua ambayo inalenga kudhoofisha uchumi wa Iran ambao unategemea zaidi mauzo ya mafuta kwa mataifa kama China, Uturuki, Iraq, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), na India.
Ubalozi wa China mjini Washington umekosoa vikali mbinu hiyo ya Trump, ukisema kuwa China itachukua “hatua zote muhimu” kulinda maslahi yake na kupinga kile walichokiita vikwazo haramu vya upande mmoja. China ndiyo mteja mkuu wa mafuta ya Iran, hivyo ushuru huo wa asilimia 25 unaweza kuzusha vita mpya ya kibiashara kati ya Washington na Beijing.
Hali nchini Iran inazidi kuwa tete huku maandamano yaliyoanza Desemba 28, 2025, yakifikia kilele cha madai ya kutaka kuanguka kwa utawala wa kidini uliopo tangu mwaka 1979. Kwa mujibu wa shirika la haki za binadamu la HRANA, kufikia sasa vifo 646 vimehakikiwa, vikiwemo vya waandamanaji 505 na maofisa usalama 113, huku watu zaidi ya 10,700 wakishikiliwa na vyombo vya dola.
Pamoja na vitisho hivyo, Serikali ya Iran (Tehran) imeeleza kuwa bado inajaribu kuweka wazi njia za mawasiliano na Washington ili kutafuta suluhu, ingawa Rais Trump tayari amebainisha kuwa yuko kwenye mawasiliano na makundi ya upinzani nchini Iran.