Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema mazungumzo yake na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, yamekuwa na tija na kwamba wamepiga “hatua kubwa” licha ya kutofikia makubaliano ya moja kwa moja kuhusu mzozo unaoendelea.
Viongozi hao wawili wamezungumza kwa pamoja jukwaani siku ya Ijumaa, Alaska, Marekani- kwa takriban dakika 10 baada ya kikao chao cha faragha, ambapo wote walionesha matumaini juu ya mazungumzo hayo.
“Hakuna makubaliano hadi maafikiano yawepo, na bado hatukufikia tulipotaka ila tumepiga hatua kubwa,” amesema Trump, akiongeza kuwa wamekubaliana juu ya masuala mengi huku machache yakisalia, yakiwemo “moja muhimu zaidi” bila kulitaja.
Kwa upande wake, Putin ameeleza kuwa ana nia ya dhati ya kumaliza mzozo huo ambao aliuita “janga”. Hata hivyo, amesisitiza kuwa Urusi inahitaji sababu za msingi za mzozo huo zitafutiwe suluhu kwanza na kuonya kuwa Ukraine na mataifa ya Ulaya “hazipaswi kuhujumu” mazungumzo hayo.
Putin ameelezea mkutano huo kama “mahali pa kuanzia kwa utatuzi” huku akisisitiza uhusiano wake na Trump kuwa ni “imara”. Amekubaliana pia na madai ya Trump kwamba vita vingeelezwa tofauti endapo angalibaki madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Trump alimalizia kwa kusema kuna uwezekano mkubwa wa kukutana tena na Putin hivi karibuni, akibainisha kuwa “mara nyingine tutakuwa Moscow,” kauli ambayo Putin aliitikia kwa kutabasamu.