Vijana nchini Tanzania wametoa wito kwa wenzao kote nchini kuitunza amani kwa wivu mkubwa na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuleta vurugu, hasa kupitia mitandao ya kijamii.
Wito huo umetolewa wakati vijana mbalimbali walipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu athari za maandamano ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na kusababisha taharuki katika maeneo kadhaa nchini.
“Tusiruhusu Machafuko Yaturejee”


Vijana hao wamesema matukio hayo yameathiri maisha ya wananchi wengi, biashara, na usalama kwa ujumla, wakisisitiza kuwa machafuko si suluhisho la changamoto zozote za kijamii au kisiasa.
“Taharuki za watu zimekuwa nyingi. Watu wamekosa amani, familia zimepoteza wapendwa, na biashara nyingi zimeporomoka kwa sababu ya hofu. Haya mambo hatuyahitaji tena,” amesema kijana mmoja.
Mitandao ya Kijamii Itumike Kujenga, Siyo Kubomoa
Vijana hao wameonya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwa ajili ya uchochezi na kusambaza taarifa za upotoshaji, wakisema teknolojia hiyo inapaswa kutumika kukuza uchumi na maendeleo ya kijamii.
“Mitandao ya kijamii siyo kwa fujo. Tumie mitandao kwa kazi, biashara, elimu na ubunifu ili maisha yaendelee. Uchochezi hautusaidii kitu,” alisisitiza kijana mwingine.
Wito wa Elimu kwa Vijana
Aidha, vijana hao wameomba Serikali na taasisi mbalimbali kuongeza elimu kwa vijana kuhusu utamaduni wa amani, maadili ya uraia, na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.
“Mara nyingi vijana tunaonekana kama tatizo, lakini wengi hatuna elimu ya kutosha kuhusu namna ya kushiriki katika mabadiliko ya amani. Tunaomba Serikali itupe elimu ili tuwe wabunifu, si wachochezi,” amesema mmoja wa vijana.