Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limeweka sheria na kanuni kali zinazosimamia mchezo huo namba moja pendwa Duniani, ambapo miongoni mwa sheria na kanuni hizo ni zile zinazotenganisha soka na siasa, na iliweka hivyo ikiamini kwamba mchezo huo utafanya vizuri zaidi ukiwa unajiendesha kwa uhuru pasipo kuegemea upande wowote miongoni mwa pande mbili au zaidi zisizokubaliana kutokana na tofauti za itikadi za kisiasa
Kwa kufanya hivyo, mchezo wa soka Duniani kama ilivyokuwa michezo mingine umekuwa kinara wa kuunganisha na kukutanisha pamoja makundi ya aina tofauti ambayo kwenye mazingira ya kawaida yamekuwa yakitofautiana kwenye itikadi na mitazamo ya kisiasa, kidini, kijamii, kitamaduni nk, na kwamba katika kusimamia hilo FIFA imekuwa haina simile kwa klabu/ timu, shirikisho la soka la nchi au Bara, viongozi wa soka na hata serikali zinazojaribu kuingilia masuala ya soka kwa namna moja au nyingine
Miongoni mwa sababu za kuchukua msimamo huo ni kulinda uadilifu wa mashindano ikiwa siasa zitaingilia kati, timu au wachezaji wanaweza kuchaguliwa, kuadhibiwa, au kupendelewa kwa sababu za kisiasa badala ya uwezo wa michezo, kwani FIFA inataka mechi ziamuliwe kwa ujuzi na uchezaji wa haki, si kwa ajenda za kisiasa.
Katika kuepuka ubaguzi na mgawanyiko unatokana na migogoro ya kisiasa, FIFA inaamini ikiruhusu siasa kuchukua nafasi kwenye soka inaweza kugawanya mashabiki au kuleta mazingira ya uhasama miongoni mwao, hivyo kuamua kubaki upande wa kati, ikumbukwe kuwa FIFA inalenga kuyafanya viwanja na mashindano yawe wazi kwa kila mtu bila kujali imani za kisiasa au utaifa
Katika kulinda taswira ya soka ni wazi kuwa kuhusisha soka na mapambano ya kisiasa kunaweza kuharibu sifa yake kama mchezo wa furaha na wa wote, FIFA inataka soka liwe jukwaa la kubadilishana tamaduni, si chombo cha propaganda au migogoro
Kwa ufupi, FIFA inaona siasa kama tishio kwa ushindani wa haki, umoja wa Dunia na upekee wa mchezo huo, hivyo inaweka sheria zinazojaribu kulifanya soka libaki kuwa ‘mchezo pekee’, ingawa kwa uhalisia siasa huendelea kujipenyeza kwa njia tofauti zisizo za uwazi
Yapo mataifa kadhaa yaliyowahi kuadhibiwa kutokana na kuhusianisha siasa/serikali na mpira
Itakumbukwa kuwa mwaka 2022 Kenya ilifungiwa kushiriki soka la kimataifa bila kikomo kutokana na serikali nchini humo kulivunja shirikisho la mpira wa miguu la nchi hiyo (FKF) na kuteua kamati maalum ya kusimamia mpira nchini humo, jambo ambalo ni kinyume kabisa na sheria na kanuni/ taratibu zinazosimamia ‘kabumbu’
Mfano mwingine ni wa nchi ya Nigeria, ambayo ilisitishwa kushiriki katika soka la kimataifa kutokana na serikali ya nchi hiyo kulisitisha Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) baada ya kombe la Dunia, ikiwashutumu maafisa wake kwa ufisadi
Hivyo, FIFA wanakuwa wakali zaidi pale wanapobaini siasa kuingilia masuala ya soka, na endapo siasa ikiwa na nafasi katika mpira itaunyima mpira uhuru wake na mpira huohuo utatumika kama sehemu ya kupenyeza ajenda za kisiasa;
Msingi wa makala hii ni baadhi ya matukio yaliyojitokeza nchini katika kipindi cha hivi karibuni ambapo fikira zangu zinanituma kwamba endapo kama Taifa tusipoongeza umakini kwenye masuala yahusuyo soka, sheria, kanuni na taratibu zake basi huenda ikawa ni rahisi siku moja isiyokuwa na jina tukaona Watanzania hususani wapenzi wa mchezo huo pendwa namba moja Duniani, na kila tunachofanya kwenye eneo hilo tunapaswa kutambua kuwa soka ni utambulisho wa nchi yetu kwenye sekta ya michezo ambapo hadi sasa ligi yetu (NBC Premiere League) ni ya tano kwa ubora barani Afrika
Agosti 12.2025 Chama cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa na tukio la ‘CCM Dinner Gala’ lililofanyika Mlimani City, jijini Dar es Salaam likilenga kuendesha harambee ya kukusanya shilingi za kitanzania Bilioni 100 kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, na ikumbukwe kuwa kwa sasa hapa nchini mchakato huo wa kisiasa na Kikatiba umeshika kasi haswa, sasa pamoja na mambo mengine miongoni mwa waliojitokeza katika tukio lile la CCM ni mfanyabiashana na mwekezaji Ghalib Said Mohammed (GSM) ambaye ni Rais wa Makampuni ya GSM Group Ltd aliyeambatana na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM Mhandisi Hersi Said
Mshereheshaji alipotaka kusikia mchango kutoka kwa kampuni ya GSM alisimama Mhandisi Hersi na kusema, “taasisi ya GSM imeshaweka kwenye akaunti za Chama cha Mapinduzi shilingi bilioni 10″, akaongeza “klabu ya Young Africans na yenyewe itatoa shilingi milioni 100”, mshereheshaji akachombeza kwa kusema ‘sijasikia vizuri’ na Mhandis Hersi akarudia “Young Africans itachangia shilingi milioni 100”
Inafahamika kuwa Mhandisi Hersi ni Rais wa Young Africans SC (Yanga SC), lakini pia ni jambo lisilotiliwa shaka kuwa huyu ni ‘Kada mtiifu’ wa CCM, kuonekana kwake pale wala haikushangaza kwakuwa yeye ni mwanachama na lile ni tukio linalohusu chama chake, isingeshangaza pia kama aliposimama angeishia kutaja mchango wa GSM tu kwakuwa kila mmoja anajuwa kuwa yeye ni ‘mwajiriwa’ wa kampuni hiyo, sintofahamu imekuja pale tu alipoihusisha Yanga SC kwenye masuala ya CCM
Tamko la Mhandisi Hersi kueleza kuwa klabu anayoiongoza itachangia fedha kwa chama cha siasa limetafakarisha wengi sana na ni dhahiri ni kinyume kabisa na sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia mchezo wa soka Duniani chini cha FIFA
Yanga SC sio klabu ya wanachama au wafuasi wa CCM pekee, Yanga SC ina wanachama wanaochangia fedha zao kwa njia mbalimbali ikiwemo kulipia kadi za uanachama na mashabiki, kununua bidhaa mbalimbali kama vile jezi, kuingia viwanjani nk ili tu kuiunga mkono timu yao, lakini ikumbukwe ndani ya wanachama na wafuasi hao kuna wanachama wa vyama tofauti vya siasa, dini, kabila na wanaotofautiana kwenye maeneo mengi kabisa lakini kupitia soka wameunganishwa na Yanga SC, kitendo cha Yanga SC kuichangia CCM maana yake hela za watu hao wote zimeenda CCM hata wale ambao hawaipendi CCM, na hata wale wanaoiunga mkono CCM na Yanga SC kwa pamoja sidhani pia kama wanaweza kukubali kusikia kuwa michango yao waliyoitoa kwa klabu yao inaenda kugharamia shughuli za chama cha siasa, hivi Mhandisi Hersi aliwaza athari hasi za tangazo lile alilotoa kwa umma?, ni dhahiri amewakosea wanachama na wafuasi wa Yanga SC na ameukosea sana mpira kwa ujumla wake
Ni wazi kuwa athari ya jambo hilo imeanza kujitokeza dhahiri kwa wanachama na wafuasi wa Yanga SC, wapenzi wa soka na hata wale ambao si wapenzi wa soka lakini hawakubaliani na CCM, wameibuka kwa kasi kuhoji na kukosoa hatua hiyo iliyochukuliwa na Yanga SC, huku tukishuhudia wengine wakienda mbali zaidi kwa kuanza kuchoma bidhaa zitokanazo na klabu hiyo walizokuwa wamenunua kwa gharama zao ikiwemo jezi na hata kadi za uanachama, wengine wameenda mbali zaidi kwa kuanza ‘kuripoti’ taarifa hizo kwenye mamlaka mbalimbali za soka Barani Afrika (CAF) na Ulinmwenguni (FIFA) kupitia mitandao ya kijamii wakitaka vyombo hivyo vya kimataifa kuimulika Yanga SC na Tanzania kwa ujumla juu ya nafasi ya siasa kwenye mpira wetu, hili si jambo la kudharau hata kidogo, hili ni hatari sana kwa mustakabali wa mpira wetu
Nimeiona taarifa ya ‘ufafanuzi’ ya Yanga SC kuhusiana na jambo hilo, siwezi kutumia muda mrefu hapa kueleza kuhusu msingi wa barua hiyo kwa sababu ukweli ni kama imezidi ‘kuivua’ nguo klabu kwa kuanza kupindisha hoja iliyozungumzwa ‘public’ na kiongozi Mkuu wa klabu hiyo (Rais Hersi Saidi), jambo pekee nililolichukua na naweza kulipongeza ni suala la kuomba msamaha kwa wote waliokwazika na jambo hilo
“Mchango ule ulitolewa na taasisi ya GSM Foundation iliyo chini ya mdhamini na mfadhili wa klabu yetu Ghalib Said Mohammed na sio kupitia hela za wanachama au kutoka kwenye mfuko wa klabu, kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato”, imeeleza sehemu ya taarifa ya ‘ufafanuzi’ ya Yanga SC iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu wake Andrea Mtine
Swali la kujiuliza hapa, Rais wa Yanga SC Mhandisi Hersi Saidi kwenye matamshi yake alisema fedha inatoka kwenye taasisi ya GSM?, au alisema taasisi hiyo inaitolea Yanga SC fedha?, jibu ni hapana kwani alisema taasisi ya GSM itatoa bilinoni 10 na klabu ya Yanga itatoa milioni 100, hili ni doa ambalo dhahiri linaweza kuathiri soka letu kama CAF au FIFA wakiamua kufuatilia na kuchunguza
Hii si mara ya kwanza kuona viashiria vya siasa/serikali kuingilia mpira vikichomoza nchini, tunaweza kudharau sasa lakini wahenga walisema ‘mdharau mwiba, guu huota tende..”, tukio lingine la mpira wetu ambalo linadaiwa kuhusishwa na siasa ni mchezo wa ‘Derby ya Kariakoo’ unaohusisha Yanga SC na Simba SC, uliopaswa kuchezwa Machi 8.2025 lakini uliahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) kisha mchezo huo kupangwa tena kufanyika Juni 15.2025 lakini baadaye iliahirishwa tena na kuhamishiwa tarehe Juni 25.2025, siku ambayo ‘ilifana’
Lakini ilikuaje mchezo huo usichezwe tarehe 15 Juni ambapo Simba SC ilisema inatambua tarehe hiyo huku Yanga wakikataa, bila shaka wengi wanakumbuka kuhusu msemo maarufu wa ‘hatuchezi’, na wakaweka masharti wakishinikiza kujiuzulu kwa CEO wa Bodi ya Ligi, kuvunjwa kwa Bodi ya ligi, kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) nk, masharti ambayo yalionekana kuwa magumu na yasyotekelezeka kwenye mazingira ya kawaida hadi tarehe 13.2025 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokutana na viongozi ‘waandamizi’ wa klabu za Simba SC na Yanga SC Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma
Ghafla tu baada ya tukio lile tulishuhudia baadhi ya yale mapendekezo ya Yanga SC yakitekelezwa ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Steven Mguto aliandika barua ya kujiuzulu na CEO wa Bodi ya ligi alisimamishwa kazi, japo haikusemwa wazi kwamba ni msukumo wa kisiasa na ingawa haikuelezwa nini hasa ambacho Rais Dkt. Samia aliteta na ‘vigogo’ wa klabu hizo kongwe nchini lakini fikra za wengi hadi sasa wanaamini kwamba tukio la kukutana kwa viongozi wa vilabu hivi viwili na Rais ndiyo lililopelekea hatua hizo, inakuwaje jambo ambalo lilionekana kuwa ‘mfupa ngumu’ ghafla tu mambo yabadilike?, hapa napo ‘kelele’ za chinichini zilianza kusikika kuhusu nafasi ya siasa/ serikali kwenye mpira wetu
Tukio la mwisho katika mifano yangu ya leo ingawa sio mwisho kwa umuhimu linaresha sakata la mgogoro wa kiuongo wa Azam FC na Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Feisal Salum Abdallah (Fei Toto) na iliyokuwa klabu yake hapo awali (Yanga SC), sakata hili lilikuwa mfupa mgumu hasa na ilionekana dhahiri kama vile majawabu ya kawaida yanashindikana kutokana na ‘ngumu’ iliyokuwa inawekwa na kila upande lakini ghafla tu mambo yalibadilika
Juni 05.2022 Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alikutana na viongozi, wachezaji na Benchi la Ufundi la Yanga SC sambamba na wadau wengine wa Soka Ikulu, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya hafla ya kuwapongeza Yanga SC kufuatia kucheza fainali ya kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) ambapo pamoja na mambo mengine katika hotuba yake Rais Dkt. Samia alinukuliwa akisema, “viongozi wa Yanga SC nina ombi moja, ishu ya Fei toto (Feisal Salum Abdallah) kaimalizeni”, katika mazingira yasiyotarajiwa usiku huohuo ikiwa ni saa chache baada ya kutoka Ikulu Yanga SC ilitoa taarifa kwa umma kuwa imemuuza ‘Fei Toto’ Azam FC
Kwa muda mrefu wakati sakata miongoni mwa pande hizo mbili lingali linaendelea yalikuwepo madai kwamba nyota huyo alishawishiwa kuvunja mkataba wake na Yanga SC, ushawishi uliodaiwa kutoka kwa ‘vigogo’ wa Azam FC, ingawa hakuna uhakika wa moja wa madai hayo lakini kitendo cha Yanga SC kutangaza kufanya biashara na matajiri hao wa Chamazi ghafla kiliacha maswali lukuki kuhusu umalizwaji wa sakata hilo, na kuhusika kwa Azam FC
Sio dhambi klabu kumshawishi mchezaji kujiunga nao, lakini pale anaposhawishiwa kinyume na taratibu hapo mamlaka za soka Duniani zimeweka adhabu kali sana, hata hivyo licha ya kwamba kauli ya Rais Dkt. Samia kwa Yanga SC kuhusiana na sakata la Feisal lilikuwa ni ombi, lakini ni upo ukweli usiokuwa rasmi kwamba ‘ombi la Rais wa Nchi ni agizo’
Tafakuri yangu kwenye makala hii, inamaliza kwa kutoa tahadhari kubwa kwa wadau wa soka Nchini, kila mmoja kwa nafasi yake atafakari mustakabali wa soka letu, wanasema ‘bandu bandu humaliza gogo’, na ‘chovya chovya humaliza buyu la asali’, au pengine tuseme ‘mdharau mwiba guu huota tende’, kama tunaupenda mpira wetu basi tujitafakari endapo tunauendesha kwa kufuata misingi ya Sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia soka Duniani au tuna busara zetu?.