Latest Posts

UBORA WA KOROSHO CHANGAMOTO KWA WABANGUAJI WADOGO MTWARA

Upatikanaji wa soko na ubora wa korosho ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wabanguaji wadogo wa zao hilo mkoani Mtwara, hali inayosababisha malalamiko ya uhaba wa wanunuzi.

Changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na matumizi ya mashine za mkono (manual) zenye ufanisi mdogo hivyo Ili kukabiliana na hali hiyo Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imejipanga kutatua changamoto za wabanguaji wadogo kuanzia kwenye ubora, masoko, na kiasi kinachobanguliwa kwa lengo la kufanikisha dhamira ya kubangua korosho zote nchini ifikapo mwaka 2030.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa CBT Francis Alfred, Septemba 8, 2025 wakati wa ziara ya Balozi wa Urusi nchini Tanzania Andrey Avetisyan, katika eneo la mradi wa ujenzi wa Kongani ya Viwanda kijiji cha Maranje Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara.

Alfred amesema kuwa kwa msimu wa 2025/2026 bodi itagawa mashine za umeme zisizopungua 50 zenye uwezo wa kubangua tani 500 kwa siku ili kuwawezesha wabanguaji wa ndani kuachana na mashine za mkono.

Aidha, amebainisha mpango wa kuwawezesha wabanguaji hao kupitia kuanzishwa kwa vituo maalum vya kuuza korosho karanga ambapo majaribio tayari yameanza kwa vikundi 20.

Kwa upande wake Balozi Avetisyan ameonesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kongani hiyo na kuahidi kuitangaza fursa hiyo nchini Urusi ili manufaa yaende kwa pande zote mbili.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala, amesema ziara ya balozi huyo ni ishara ya urafiki wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Urusi hususan katika uwekezaji wa kilimo ambao umechochewa na juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!