Na Vanessa Sindato.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz wameeleza dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zao, wakizingatia changamoto za kisiasa zinazolikumba bara la Ulaya na dunia kwa ujumla.
Kulingana na taarifa ya DW inasema, kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya ujerumani Stefan Kornelius, Merz na Marcon wamejadiliana kuhusu suluhisho la mvutano unaozingira mradi wa ndege za kivita wa FCAS unaojumuisha Ujerumani, Ufaransa na Uhispania, ambapo wamekusudia kufikia makubaliano kabla ya mwisho wa mwezi Agosti.
Mradi huo wa thamani ya zaidi ya yuro bilioni 100 umekuwa ukikwamishwa na mgogoro wa muda kuhusu masuala ya uundaji na umiliki wa teknolojia husika.
Pia, mazungumzo yao yalijumuisha masuala mapana yanayogusa sera za Ulaya, mzozo wa Ukraine, na hali ya Mashariki ya Kati.
Viongozi hao walijadili kwa kina mustakabali wa mahusiano ya kiuchumi kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani, kufuatia tishio la Rais Donald Trump kutaka kuanzisha ushuru wa asilimia 30 kwa bidhaa kutoka Ulaya iwapo makubaliano ya kibiashara hayatapatikana kabla ya Agosti mosi.