Urusi imeanza kuwaondoa maafisa wake wa kijeshi kutoka Burkina Faso ili kuwasaidia katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
Kwa mujibu wa BBC Swahili, maafisa wapatao 100 kutoka Bear Brigade, kampuni ya kijeshi binafsi ya Urusi, ni miongoni mwa wanajeshi 300 waliopelekwa katika taifa hilo la Afrika Magharibi mwezi Mei ili kusaidia jeshi la Burkina Faso kukabiliana na wapiganaji wa itikadi kali katika Waislamu.
Katika taarifa iliyotolewa kupitia chaneli yao ya Telegram, kundi hilo la Bear Brigade lilieleza kuwa vikosi vyake vinarejea nyumbani kusaidia kulinda Urusi dhidi ya mashambulizi ya Ukraine katika eneo la Kursk.
Hata hivyo, hatua hii ya Urusi imeibua wasiwasi kuwa inaweza kuwatia moyo wapiganaji wa Kiislamu nchini Burkina Faso, ambao wamekuwa wakihusika na mashambulizi mabaya katika miaka ya hivi karibuni.
BBC Swahili iliripoti kuwa mashambulizi hayo yameua hadi watu 300 hivi karibuni, katika moja ya matukio makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini humo.
Tangu mwaka 2015, Burkina Faso imekumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya wanajihadi, hali iliyopelekea zaidi ya watu milioni mbili kuyakimbia makazi yao. Hili limezidisha changamoto kwa jeshi la nchi hiyo, ambalo liko chini ya uongozi wa Rais wa mpito, Kapteni Ibrahim Traoré, aliyeingia madarakani kwa mapinduzi mnamo Septemba 2022.
Licha ya jitihada za kutafuta ushirikiano mpya wa usalama na Urusi, serikali ya Burkina Faso bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya kudhibiti karibu nusu ya nchi ambayo ipo nje ya udhibiti wake.
Miongoni mwa mashambulizi ya hivi karibuni, shambulio la kinyama lililotokea siku ya Jumamosi katika mji wa kaskazini wa Barsalogho liliripotiwa kusababisha vifo vya takribani watu 300, kwa mujibu wa walionusurika. Shambulio hilo linadaiwa kufanywa na kundi la wanamgambo lenye mafungamano na al-Qaeda, Jamaat Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM).
Serikali ya Burkina Faso haijatoa takwimu kamili za waliouawa, lakini Waziri wa Mawasiliano, Rimtalba Jean Emmanuel Ouedraogo aliliita tukio hilo kuwa la kinyama.
Raia na wanajeshi waliokuwa wakichimba mitaro kwa ajili ya kulinda mji huo dhidi ya mashambulizi ya wanajihadi walikuwa miongoni mwa wahanga wa shambulio hilo.