Jeshi la Polisi nchini limekanusha vikali uvumi uliosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kupatikana kwa kontena lililosheheni silaha katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 1, 2025 Jijini Dodoma Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna Msaidizi wa Polisi (DCP) David Misime, amesema kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote na zina lengo la kupotosha umma pamoja na kuleta taharuki isiyo ya lazima.
Aidha Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama nchini ni shwari, na kwamba mipaka yote ya nchi inalindwa kikamilifu huku akiwaomba wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa njia sahihi, kuepuka kusambaza taarifa zisizothibitishwa, na kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.
Taarifa hizo Zilizokanushwa na Jeshi la Polisi Nchini zilizosambaa katika mitandao ya kijamii Mara baada ya Mwanamtandao Mange kimambi kuzichapitisha kupitia mitandao yake ya Kijamii zikieleza kuingizwa kwa silaha za kivita Nchini.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa ufafanuzi kuhusu matukio ya utekaji na kupotea kwa watu ambayo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara katika vituo vya polisi ambapo kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa kwa kina, imebainika kuwa si matukio yote yanayotokana na uhalifu wa kweli, bali mengine yamekuwa yakisababishwa na sababu binafsi au za kijamii
Misime, amesema kuwa baadhi ya matukio hayo yanatokana na watu kujiteka wenyewe, wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, migogoro ya kugombea mali, pamoja na nia ya kulipiza kisasi.
Aidha (DCP) Misime amesema kuwa jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa kina katika kila tukio linaloripotiwa, ili kuhakikisha ukweli unajulikana na hatua stahiki zinachukuliwa. Aidha, amewaasa wananchi kuacha kutumia njia za udanganyifu au kuchukua sheria mikononi mwao, na badala yake kushirikiana na vyombo vya dola katika kutatua migogoro na matatizo yao.