Latest Posts

VIJANA KENYA WAANDAMANA WAKUMBUKA WALIOUAWA JUNI 25, WAAPA KUENDELEA KUPIGANIA HAKI

Maelfu ya waandamanaji, wengi wao wakiwa vijana, wamemiminika mitaani kote Kenya Jumatano hii kuadhimisha mwaka mmoja tangu siku ya umwagaji mkubwa wa damu ilipotokea wakati wa maandamano ya kupinga serikali, huku hofu ya kushambuliwa na makundi ya wahuni wanaodaiwa kuungwa mkono na dola ikitanda.

Juni 25, 2024 iliacha alama ya majonzi katika historia ya taifa hilo baada ya wananchi kuvamia Bunge la Taifa jijini Nairobi wakiandamana dhidi ya kupanda kwa kodi na hali ngumu ya maisha. Takribani watu 60 waliuawa na maafisa wa usalama katika maandamano hayo yaliyodumu kwa wiki kadhaa.

Mwaka mmoja baadaye, waandamanaji wamejitokeza kuwakumbuka waliopoteza maisha, wakiwa wamebeba mabango yenye picha za waathirika na kupaza sauti zao kwa kauli ya “Ruto must go” (Ruto lazima aondoke). Waandamanaji wengi wakiwa vijana waliokuwa wakipeperusha bendera za Kenya, walikusanyika licha ya tahadhari kwamba serikali ingetumia mbinu kali kuwazuia.

“Nimekuja hapa kama kijana wa Kenya kuandamana, ni haki yetu kwa ajili ya wale wenzetu waliouawa mwaka jana. Polisi wapo hapa lakini kazi yao imekuwa kutuua badala ya kutulinda,” amesema Eve, msichana mwenye umri wa miaka 24 ambaye hana ajira, alipoongea na shirika la habari la AFP.

Katika maeneo mengi ya Nairobi, barabara kuu zilifungwa mapema asubuhi huku majengo ya serikali yakizungushiwa nyaya zenye makali ya chuma, ikionesha maandalizi dhidi ya uwezekano wa uvunjifu wa amani. Biashara na shule nyingi zilibaki zimefungwa.

Baadhi ya wanaharakati walitoa wito wa “#OccupyStateHouse” wakitaka maandamano ya kuhamia Ikulu ya Nairobi kama njia ya kuonesha hasira yao kwa Rais William Ruto, huku kukiwa na kumbukumbu ya wito kama huo mwaka jana uliopelekea mashambulizi makali na mauaji ya raia.

Angel Mbuthia, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Jubilee cha upinzani, amesema: “Ni muhimu sana kwa vijana wa Kenya kuadhimisha Juni 25 kwa sababu waliopoteza maisha walikuwa vijana kama wao – waliokuwa wanapigania utawala bora.”

Lakini hali ya sintofahamu iliendelea kutanda kufuatia kifo cha hivi karibuni cha mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang’ aliyefariki mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kumkosoa afisa mwandamizi wa usalama. Taarifa za uchunguzi zinaeleza kuwa aliteswa na kufariki kutokana na kipigo, ingawa polisi walidai alijiua.

Polisi wamesisitiza kuwa maandamano yanaruhusiwa ilimradi ni “ya amani na bila silaha.” Hata hivyo, ripoti za waandamanaji kushambuliwa na vikundi vya “goons” (wahuni wanaotumia pikipiki na silaha za jadi kama mijeledi na marungu), ambao hudaiwa kufanya kazi kwa ushirikiano na polisi, zimezusha taharuki.

Katika taarifa ya pamoja, ubalozi wa Marekani, Uingereza na Ujerumani nchini Kenya wamelaani matumizi ya wahuni kwa lengo la kutatiza mikusanyiko ya amani.“Tunalaani vikali matumizi ya wahuni wa kukodiwa ili kuvuruga au kushambulia maandamano ya amani,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!