Latest Posts

VIJANA TARIME KUNUFAIKA NA MPANGO WA CHIFU ZAKARIA

Na Fredrizzo Samson, Mara

Chifu wa kabila la Kurya, koo ya Watimbaru Inchage, Chifu Peter Zakaria, ameanzisha mpango maalum wa kukutana na makundi mbalimbali ya vijana wilayani Tarime kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kuweka mikakati ya pamoja ya kuwawezesha kiuchumi na kijamii.

Mpango huo unatajwa kuhusisha viongozi wa kata na mitaa, Jeshi la Polisi pamoja na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini.

Katika awamu ya kwanza, Chifu Zakaria amekutana na vijana wa kata tatu ambazo ni Nyamisangura, Sabasaba na Turwa, zote zilizopo ndani ya Jimbo la Tarime Mjini, huku akibainisha kuwa mikutano itaendelea katika kata nyingine kulingana na ratiba iliyopangwa.

Kikao hicho kilichofanyika katika kumbi ndogo za CMG Hotel, kililenga kusikiliza changamoto zinazowakabili vijana wa Tarime na kujadili namna ofisi ya Chifu, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ndani na nje ya wilaya, inaweza kushiriki kuwainua vijana hao.

Katika kikao hicho, vijana waliwasilisha hoja mbalimbali, ambapo ukosefu wa ajira ulitajwa kuwa changamoto kubwa inayosababisha baadhi yao kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani, wizi, ukabaji pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya na pombe haramu maarufu kama “vinusu”.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime–Rorya, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo Mark Njera, aliyewakilishwa na Operation Officer wa Mkoa wa kipolisi Tarime-Rorya, Festo George Ukulule, alisikiliza hoja za vijana na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii na Jeshi la Polisi katika kulinda amani na usalama wa Tarime na Mkoa kwa ujumla.

Katika maelezo yake, ulinzi shirikishi ulitajwa kuwa nyenzo muhimu ya kukabiliana na uhalifu mitaani, huku Jeshi la Polisi likihimizwa kuratibu zoezi hilo kwa karibu kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa.

Akijibu hoja zote, Chifu Zakaria alitangaza mpango wa kuandaa harambee kabambe itakayowahusisha wadau wa maendeleo na marafiki kwa lengo la kukusanya fedha zitakazotumika kuwawezesha vijana kujiajiri.

Alieleza kuwa fedha hizo zitatumika kununua mashine za kuoshea magari, mashine za kujazia upepo kwenye magurudumu ya vyombo vya moto, pamoja na pikipiki zitakazotolewa kwa vijana kwa masharti nafuu na marejesho madogo.

Aidha, Chifu Zakaria aliwataka vijana kuheshimu maadili, kushikamana na kulinda amani ya Tarime na Mkoa wa Mara kwa ujumla, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo na ikipotea ni vigumu kuirejesha.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!