Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Bi. Mary Maganga, amewataka vijana kote nchini kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kuchagua viongozi wanaoakisi matumaini, dira na ndoto za taifa la Tanzania katika miaka mitano ijayo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Vijana Tanzania, linalofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa City Park Garden jijini Mbeya na kuhudhuriwa na vijana zaidi ya 1,500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Bi. Maganga amesema vijana wana nafasi ya kipekee katika mabadiliko ya kijamii na kiuchumi ya taifa.
“Vijana ni nguvu ya mabadiliko na maendeleo katika jamii zetu. Hivyo ni lazima tutumie vyema nguvu hii kubadilisha dunia kuwa mahali bora kwa ajili ya watu wote. Ninawasihi mjitokeze kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, na kuchagua viongozi wenye dira sahihi kwa taifa letu,” amesema Bi. Maganga.
Amefafanua kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mikakati ya kuwawezesha vijana kupitia mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi, sambamba na programu za uwezeshaji kiuchumi zinazolenga kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya taifa.
Amesema serikali imejikita katika kuimarisha ajira, ubunifu na ujasiriamali kwa vijana, hivyo ni wakati wao wa kutumia sauti yao ipasavyo, hasa kupitia kura zao, ili kuimarisha msingi wa maendeleo wa taifa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Rodrick Mpogolo, amewataka vijana kuendelea kuwa wazalendo na kujivunia taifa lao, akisema mchango wao ni muhimu katika kulijenga taifa lenye misingi imara ya maendeleo.
Amesema kijana mzalendo ni yule anayeitumikia nchi yake kwa uadilifu na upendo na kwamba nchi hii inawategemea vijana katika kulinda amani na kuendeleza maendeleo.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Ofisi ya Waziri Mkuu, Seleman Mvunye, amesema kongamano hilo limekusudia kujenga uelewa, kubadilishana mawazo na kuwajengea uwezo vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa manufaa ya taifa.