Vijana wametahadharishwa dhidi ya maudhui ya baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii, wakitakiwa kuwakataa na kujitenga na wale wote wanaohamasisha vurugu, ghasia na chuki miongoni mwa Watanzania, wakitakiwa kuwa makini katika kuchuja yale yaliyopo kwenye mitandao ya Kijamii.
“Wapo Vijana wanaojiweka kwenye makundi na kufuata yale wanayoyaona kule kwenye Tiktok, Instagram na WhatsApp, mimi niwaombe wasiwafuatilie maana wanataka kutugombanisha sisi watanzania ikiwa huna ajira nikuombe uje tuendeshe bodaboda, tuuze nguo na kadhalika ili kujipatia kipato na tuachane na hao wasiotutakia mema sisi wananchi.”
Wito huo umetolewa na Bw. Alex Vitalis Ndailagiji, Kijana na Afisa usafirishaji kwa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda, wakati akizungumza kuhusu ghasia, wizi na matukio ya uharibifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akieleza namna ambavyo aliathirika na matukio hayo kiuchumi na kijamii.
Ndailagiji amewasihi watanzania kutokubali mitandao ya kijamii ikatumika kuwagombanisha na kuwakwamisha kiuchumi, akiwataka Vijana kushiriki pamoja katika ujenzi wa Taifa lao badala ya kuwa sehemu ya kuharibu na kuiba mali za umma na za watu binafsi.
Ndailagiji ameeleza pia kukosa uhalali kwa maandamano ya Oktoba 29, 2025, akisema hakufurahishwa nayo na hayaungi mkono kutokana na namna yalivyotumika kama kivuli cha kuiba, kuharibu na kuua raia na kuharibu maisha ya watu wengine kiuchumi na kijamii.