Vijiji 160 katika mikoa ya Iringa, Ruvuma, Njombe na Lindi vinatarajiwa kunufaika na mpango wa matumizi bora ya ardhi utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka minne, kufuatia Mradi wa FORLAND kuingia makubaliano ya utekelezaji na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC).
Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha upangaji shirikishi wa matumizi ya ardhi katika ngazi ya vijiji, kupunguza migogoro ya ardhi pamoja na kulinda rasilimali za asili hususan misitu.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika mjini Iringa, Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Joseph Mafuru, amesema mipango ya matumizi bora ya ardhi imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kupunguza na kudhibiti migogoro ya ardhi nchini.

Mafuru ameeleza kuwa hadi sasa zaidi ya vijiji 4,000 tayari vimepimwa na kuandaliwa mipango ya matumizi bora ya ardhi, hatua iliyosaidia kuweka mipaka wazi, kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi na kupunguza migogoro kati ya wakulima, wafugaji na wawekezaji.
Kwa upande wake, Mshauri Mkuu wa Mradi wa FORLAND, Michael Hawkes, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuimarisha upangaji endelevu wa matumizi ya ardhi katika ngazi ya jamii, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi katika kila hatua ya utekelezaji.

Naye Mtaalamu wa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi kutoka Mradi wa FORLAND, Andrew Fednands, amesema lengo la ushirikiano huo si tu kupunguza migogoro ya ardhi, bali pia kuimarisha uhifadhi wa misitu na kuchangia maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika maeneo ya vijiji vinavyonufaika.
Utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto za migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini, sambamba na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za asili na kuchochea maendeleo ya wananchi katika sekta za kilimo, ufugaji na mazingira.
