Latest Posts

VYOMBO VYA HABARI KENYA VYAPIGWA ‘STOP; KURUSHA MAANDAMANO

Serikali ya Kenya imeamuru vituo vyote vya televisheni na redio nchini kusitisha mara moja matangazo ya moja kwa moja yanayohusu maandamano ya kitaifa yanayoendelea kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024 ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 60.

Katika barua rasmi iliyoandikwa kwa vyombo hivyo vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA), David Mugonyi, ameeleza kuwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano ya Juni 25, 2025 ni kinyume na Katiba na sheria za mawasiliano za nchi hiyo.

“Matangazo ya moja kwa moja ya maandamano ya tarehe 25 Juni 2025 yanakiuka Kifungu cha 33(2) na 34(1) cha Katiba ya Kenya pamoja na Sehemu ya 461 ya Sheria ya Mawasiliano ya Kenya ya mwaka 1998,” imesomeka sehemu ya barua hiyo.

Mugonyi amevitaka vyombo hivyo vya habari kusitisha mara moja urushaji wa maandamano hayo au vitarajie kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria.

“Hii ni agizo kwa vituo vyote vya televisheni na redio nchini kusitisha mara moja urushaji wa moja kwa moja wa maandamano hayo. Kushindwa kutekeleza agizo hili kutasababisha hatua za kisheria kulingana na Sheria ya Mawasiliano ya Kenya ya mwaka 1998,” ameongeza Mugonyi.

Agizo hilo limekuja wakati maandamano yakiwa yameenea katika miji mikubwa kama Nairobi, Mombasa na Eldoret, pamoja na miji ya Kakamega, Narok, Busia, Makueni, Nyeri, Laikipia, Nyandarua, Machakos, Homa Bay, na Kirinyaga.

Licha ya hatua hiyo ya serikali, maandamano yameendelea yakiongozwa na vijana waliovalia bendera za taifa, wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kutaka haki na kumbukumbu kwa vijana waliopoteza maisha yao mwaka mmoja uliopita.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!