Latest Posts

WAENDESHA MAGHALA WAASWA KUSIMAMIA UBORA WA KOROSHO KWA UADILIFU

Kuelekea msimu wa korosho wa 2025/2026, Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imeendesha mafunzo kwa wadau mbalimbali wa zao hilo ili kuhakikisha wanazingatia ubora na kuzidisha ushindani wa kimataifa.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo ya Udhibiti Ubora wa Korosho Ghafi yaliyoandaliwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Katibu Tawala wa Wilaya ya Mtwara Wakili Richard Mwalingo, ametoa maelekezo kwa washiriki kuhakikisha wanafikisha elimu kwa wakulima na  ameiahidi pia Bodi ya korosho kuwa mamlaka ya mkoa na wilaya ziko tayari kushirikiana ili kuhakikisha miongozo inatekelezwa kwa lengo la kufikia malengo ya uzalishaji wa tani milioni 1 ifikapo mwaka 2030.

Mwalingo ameongeza kuwa korosho ni moja ya mazao ya kimkakati nchini Tanzania hivyo amewataka washiriki kuweka uzalendo mbele kwa kufanya kazi kwa kusimamia kanuni na maelekezo wanayopewa katika kutekeleza majukumu yao, Aidha amesema serikali haitaweza kumvumilia mtu yeyote atakayehusika na kuhujumu ubora wa korosho.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred, amewaomba waendesha maghala waache kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia maadili na uadilifu.

Amesema ili kuendelea kubaki vinara katika sekta ya korosho ni wajibu wa kila mtu katika kitengo chake kuhakikisha anasimamia ubora wa zao hilo ikiwemo wasimamizi wa maghala kupokea korosho zenye ubora.

“Tunachopigania sisi hapa ni nchi, hatupiganii mtu mmoja bali maslahi ya taifa. Tukipeleka korosho yenye ubora wa hali ya juu inamaanisha tutaendelea kupata wanunuzi wengi kupitia Tanzania, tutaongeza ushindani, bei zitaimarika na wakulima watanufaika,” amesema Alfred.

Aidha, kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Nyaburuma Wanjara, wamesema mafunzo hayo yamewakumbusha kusimamia kanuni ili kuhakikisha ubora wa korosho unakuwa juu na kufanya pato la nchi kuendelea kukuwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!